Aug 30, 2023 08:05 UTC
  • AU kundoa askari wengine 3,000 kutoka Somalia

Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kimesema kitawaondoa wanajeshi wengine 3,000 katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Kamanda wa ATMIS, Luteni Jenerali Sam Okiding alisema hayo jana Jumane mjini Mogadishu katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, "Maandalizi ya awamu ya pili ya kuwaondoa askari 3,000 wa ATMIS nchini Somalia kufikia mwishoni mwa Septemba yanaendelea."

Kikosi hicho ambacho hapo awali kilikuwa kinajulikana kama AMISOM kiliondoa wanajeshi wake 2,000 wa kulinda amani nchini Somalia mapema mwaka huu.

Juhudi za kujenga uwezo wa kuviwezesha vikosi vya usalama vya Somalia kuchukua jukumu kamili la usalama wa nchini mwao wakati ATMIS itakapoondoka kikamilifu nchini Somalia mwezi Disemba 2024 zinaendelea.

Wanajeshi wa AU nchini Somalia

Haya yanajiri huku wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wakiripotiwa kuteka miji mitano iliyoko katikati ya Somalia. Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, magaidi hao wakufurishaji wametwaa miji ya Wabho, Osweyne, Budbud, Gal’ad, na Masagaway katika jimbo la Galmudug, baada ya wanajeshi wa Somalia kuondoka katika miji hiyo juzi Jumatatu.

Habari zaidi zinasema, genge hilo la kigaidi limeua wanajeshi 178 wa Somalia katika mapigano baina ya pande mbili hizo katikati ya Somalia. Hata hivyo halijasema idadi ya wanachama waliouawa katika makabiliano hayo.

Tags