Paris yaakiri kushindwa kwa sera zake za kikoloni barani Afrika
(last modified Thu, 07 Sep 2023 02:37:55 GMT )
Sep 07, 2023 02:37 UTC
  • Paris yaakiri kushindwa kwa sera zake za kikoloni barani Afrika

Mapinduzi mtawalia yaliyotokea katika nchi kadhaa za Kiafrika kama Niger na Gabon, ambayo amepongezwa na kupokewa kwa shangwe na wananchi, yamegeuka kuwa harakati kubwa dhidi ya ukoloni mpya na mamboleo wa Ufaransa barani Afrika.

Raia wengi wa nchi hizo ambao wamekaribisha mamageuzi ya kisiasa katika chini zao, wameunga mkono serikali mpya na kutaka kukatwa uhusiano na Ufaransa na hata kufukuzwa balozi wa nchi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Catherine Colonna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, amekiri rasmi kwamba zama za ukoloni wa nchi hiyo barani Afrika zilipita muda mrefu uliopita na kwamba kwa sasa kumeibuka wimbi la chuki dhidi ya Wafaransa barani Afrika.

Ufaransa imekuwepo katika nchi tofauti za Kiafrika kwa karne nyingi kwa visingizio mbalimbali. Jinai za kihistoria za Ufaransa nchini Algeria, ikiwa ni pamoja na mauaji ya wapigania uhuru na kufanya majaribio ya nyuklia kwa kutumia wakaazi wa baadhi ya maeneo ya Algeria kama mapanya wa maabara, ni uhalifu mkubwa ambao kamwe hauwezi kusahaulika.

Catherine Colonna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa

 

Ijapokuwa raia wa nchi mbalimbali za bara la Afrika waliweza kujiondoa kwenye makucha ya ukoloni wa Wafaransa kwa mapambano ya muda mrefu ya kupigania uhuru, lakini utajiri na hadhi ya bara hilo haikuwa jambo ambalo Wafaransa wangeweza kulifumbia macho kirahisi. Utajiri ya madini ya urani, dhahabu, almasi na kadhalika, na nafasi nzuri ya kijiografia ya nchi nyingi za Afrika, vimeifanya Ufaransa itazame upya mbinu zake za kikoloni na kupanga sera mpya kuhusu masuala yake ya kisiasa na kiuchumi barani Afrika. Kulinda usalama na mapambano dhidi ya vikundi vya kigaidi, misaada ya kiuchumi kupitia njia ya kutoa mikopo ya muda mrefu, kuanzisha kambi na vituo vya mafunzo ya kijeshi kwa askari wa nchi tofauti za Afrika, na pia msaada wa kisiasa wa nyuma ya pazia kwa baadhi ya viongozi vibaraka wa nchi mbalimbali za bara Afrika, ni miongoni mwa sera na mambo yaliyotumiwa na Ufaransa katika miongo ya hivi karibuni kwa ajili ya kuimarisha uwepo na ushawishi wake katika nchi za bara hilo.

Ripoti zilizochapishwa zinaonyesha kuwa, sehemu kubwa ya fueli ya urani inayohitajika katika vinu vya nyuklia vya Ufaransa inatoka kwenye migodi ya uranium katika nchi kama Niger. Pia, kampuni za Ufaransa zina hisa kwenye makampuni mengi ya kiuchumi katika nchi tofauti za Kiafrika. Kwa maneno mengine ni kwamba, Ufaransa inapata dhahabu yake kutoka Guinea, uranium kutoka Niger, mafuta kutoka Gabon, chuma cha kutengeneza magari kutoka Mauritania, kakao kutoka Ivory Coast, mbao kutoka Kongo, na hata wanariadha wake wanaoshinda medali za michezo ya kimataifa kutoka kwenye makoloni yake ya zamani.

Scott Ritter, afisa wa zamani wa ujasusi wa Marekani, anasema kuhusiana na suala hili kwamba: “Mapinduzi yanayotokea katika nchi za Afrika ni tishio kubwa kwa Ufaransa. Paris ina uhusiano mpana na nchi za Kiafrika, na kukatwa uhusiano huo kutakuwa na athari mbaya sana kwa uchumi wa Ufaransa. Inaonekana kwamba, Paris inapaswa kusubiri mustakabali mbaya kutokana na hasira ya Waafrika kwa sera ya Ufaransa ya baada ya ukoloni.”

Wananchi wa Afrika wamechoshwa na jinamili la Ufaransa

 

Wakati huo huo ripoti ya hivi karibuni ya "Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati ya Afrika" kuhusu matokeo ya uingiliaji kati wa kigeni katika bara la Afrika pia inaonyesha kuwa, uwepo wa askari wa Ufaransa barani Afrika, sio tu kwamba haukuweza kupunguza na kudhibiti ugaidi katika bara hilo, bali pia harakati za kigaidi zimeongezeka kwa 70% barani humo.

Inaonekana kwamba, kwa sasa kumeibuka kizazi kipya katika nchi za Kiafrika ambacho kwa mara nyingine tena na kwa uangalifu, kimesimama kukabiliana na ukoloni mamboleo wa Ufaransa kwa kutegemea ushirikiano wa kikanda na kuamini nguvu na uwezo wao wenyewe. Kizazi hiki hakistahamili tena uwepo wa viongozi tegemezi na vibaraka na kinataka uhuru halisi na kujitawala.

Ijapokuwa haionekani kwamba Ufaransa itasalimu amri kwa matakwa ya watu wa Afrika, lakini hapana shaka kuwa, mwamko na harakati ya sasa inaweza kuwa “hapana” na upinzani mkubwa dhidi ya vitendo na sera za Paris barani Afrika. Kwa maneno mengine ni kuwa, Afrika haitaki kuwa tena uwanja wa kujifaragua wa Ufaransa.

Tags