Kimbunga kikali cha Mediterrania, mafuriko yaua maelfu ya watu Libya
(last modified Tue, 12 Sep 2023 02:46:20 GMT )
Sep 12, 2023 02:46 UTC
  • Kimbunga kikali cha Mediterrania, mafuriko yaua maelfu ya watu Libya

Mamia ya watu wamepoteza maisha baada ya kimbunga kikali cha Mediterrania kupiga mashariki mwa Libya na kusababisha mvua kubwa na mafuriko.

Maafisa wa serikali ya mashariki ya Libya wamesema idadi ya walioaga dunia kwenye majanga hayo imeongezeka na kupindukia watu 2,000.

Msemaji wa Jeshi la Taifa la Libya, Ahmad Mesmari awali alisema kimbunga hicho kilichopewa jina la Daniel mbali na kusababisha watu zaidi ya 6,000 kutoweka, lakini pia kimebomoa nyumba na kuharibu miundombinu katika miji kadhaa ya mashariki mwa Libya.

Mismari ameeleza bayana kuwa, wanachama 11 wa Jeshi la Taifa la Libya LNA wametoweka baada ya kutokea janga hilo la kimaumbile. 

Video zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zinaashiria ukubwa wa athari za kimbunga hicho kilichopiga miji ya Benghazi, Sousse, Al Bayda, Al-Marj na Derna Jumapili na jana Jumatatu.

Ahmed Mohamed, mkazi wa mji bandari wa Derna, mashariki mwa Libya ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "Tulikuwa tumelala, na tulipoamka, tulikuta nyumba yetu imefurika maji."

Wahandisi wa mafuta wameiambia Reuters kuwa, bandari za mafuta za Ras Lanuf, Zueitina, Brega na Es Sidra zimefungwa kutokana na athari za kimbunga hicho.

 

Tags