Netanyahu: DRC itahamishia ubalozi wake Quds kutoka Tel Aviv
(last modified Sat, 23 Sep 2023 04:05:54 GMT )
Sep 23, 2023 04:05 UTC
  • Netanyahu: DRC itahamishia ubalozi wake Quds kutoka Tel Aviv

Waziri wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo karibuni itauhamishia ubalozi wake mjini Quds (Jerusalem) kutoka Tel Aviv.

Benjami Netanyahu alidokeza hayo jana Ijumaa katika taarifa, baada ya kukutana na Rais wa DRC, Félix-Antoine Tshisekedi pambizoni mwa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New  York.

Netanyahu ameongeza kuwa, utawala huo haramu unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina karibuni hivi utafungua ubalozi wake huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Haya yanajiri siku chache baada ya Papua New Guinea kufungua ubalozi wake mjini Quds, na kuwa nchi ya tano kufungua ofisi ya kidiplomasia katika mji huo mtukufu unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu. 

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ilikosoa vikali hatua hiyo na kuitaka serikali ya Papua New Guinea itazame upya msimamo wake hue huo wa kufungua ubalozi katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ikumbukwe kuwa, Disemba mwaka 2017 aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuwa Washington inaitambua Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel na kisha kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tel Aviv. 

Baadhi ya nchi kama Honduras, Kosovo, Guatemala na Paraguay zimefuata kibubusa sera za Washington na kuafiki suala la kuhamisha balozi zao kutoka Tel Aviv kwenda mji wa Quds, kitendo ambacho kinakiuka sheria za kimataifa. Hata hivyo Paraguay ilifutilia mbali uamuzi huo miezi minne baadaye.

Tags