Sep 28, 2023 07:47 UTC
  • Baraza la Kijeshi Burkina Faso lazima jaribio la mapinduzi

Baraza la kijeshi nchini Burkina Faso limetangaza kwamba, vikosi vya usalama na idara za ujasusi zilizima jaribio la mapinduzi Jumanne iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo imesema, “afisa wa jeshi (ambaye jina lake halikutajwa) na wenzake, walipanga kuvuruga nchi kwa nia ovu kwa kushambulia taasisi ya jamhuri na kuiingiza nchi yetu katika hali ya machafuko."

Imeongeza kuwa, baadhi ya watu wametiwa nguvuni, na msako wa kuwakamata wengine waliohusika na njama hiyo bado unaendelea.

Siku ya Jumanne iliyopita, mamia ya waandamanaji wanaounga mkono baraza la kijeshi linalotawala Burkina Faso walimiminika katika mitaa ya mji mkuu, Ouagadougou, kuonyesha uungaji mkono wao kwa baraza hilo, kutokana na uvumi wa kile kilichosemwa kuwa ni "uasi unaokaribia" dhidi ya utawala wa sasa. 

Mwezi Oktoba mwaka jana, Baraza la Kijeshi nchini Burkina Faso lilitangaza kwamba Ibrahim Traoré atachukua nafasi ya rais wa nchi hiyo na uongozi wa jeshi. 

Hatua hiyo ilichukuliwa takriban wiki moja baada ya mapinduzi yaliyoongozwa na Kapteni Traoré, ambayo yalimuondoa madarakani mkuu wa baraza la kijeshi, Paul-Henri Damiba, ambaye alikuwa akiongoza nchi hiyo tangu mapinduzi yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka huu.

Tags