Askari 8 wa Umoja wa Mataifa wakamatwa DRC kwa tuhuma za ubakaji
(last modified Fri, 13 Oct 2023 07:12:34 GMT )
Oct 13, 2023 07:12 UTC
  • Askari 8 wa Umoja wa Mataifa wakamatwa DRC kwa tuhuma za ubakaji

Askari wanane wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) wamekamatwa na kuzuiliwa kwa tuhuma za kuhusika na ubakaji na udhalilishaji wa kingono.

Duru za habari zimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa askari hao wa kofia ya buluu wa Umoja wa Mataifa wametiwa mbaroni kwa madai ya kuhusika na ukatili wa kingono.

Umoja wa Mataifa kwa upande wake umesema kuwa umepokea ripoti kuhusiana na 'kesi nzito za utovu wa nidhamu' dhidi ya askari hao wake wa kulinda amani Kongo DR.

Umoja huo umesema umeanzisha uchunguzi wa kesi hizo, ingawaje haujatamka wazi kuwa ni kesi za ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia zinazowakabili askari wake hao wanaohudumu nchini DRC.

Pasi na kutoa maelezo ya kina, MONUSCO imesema katika taarifa kuwa imewasimamisha kazi askari wake kadhaa wa kulinda amani nchini DRC, kwa ukosefu wa maadili.

Maandamano ya Wakongomani dhidi ya MONUSCO

Haya yanajiri wakati huu ambapo mjadala kuhusu kuondoka kwa ujumbe huo wa UN wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) ukiendelea.

Wananchi wa Kongo wamekuwa wakiandamana wakikilalamika kwamba, makundi yanayobeba silaha yangali yanaendeleza hujuma mashariki mwa nchi hiyo na kwamba kikosi hicho cha UN hakiwalindi raia.

Akihutubia hivi karibuni katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi alitoa mwito wa kutekelezwa kwa ombi la nchi hiyo la kuongeza kasi ya kuondoka kwa askari wa MONUSCO nchini DRC.

 

Tags