Sheikh Hemedi Jalala: Walimwengu wanapaswa kupinga ukandamizaji dhidi ya Wapalestina
Walimwengu wametakiwa kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na kupaza sauti za kupinga dhulma, unyanyasaji na mauaji yanayofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.
Wito huo umetolewa na Sheikh Hemedi Jalala mmoja wa viongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Tanzania wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds hapo jana jijini Dar es Salaam. Sheikh Jalala ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Imam Swadiq AS jijini Dar es Salaam amesema kuwa, Umoja wa Mataifa na viongozi mbalimbali wa dini wanapaswa kuunga mkono mapambano dhidi ya unyanyasaji, dhuluma, ukandamizaji na uonevu unaofanyika katika nchi mbalimbali ikiwemo Palestina.
Sheikh Hemedi Jalala amesema kuwa kila mpenda amani na haki bila kuangalia dini anatakiwa kwa njia moja ama nyingine kuungana kupinga ukandamizaji unaofanyika katika maeneo mbalimbali ukiwemo ule unaofanywa na Israel dhidi ya wananchi wa Palestina. Aliongeza kuwa kama ilivyo kwa watanzania ambao wanaelezwa kuwa Tanzania ni nchi yao, basi watu wote watambue kuwa Palestina ni ya Wapalestina na kusisitiza kuwa, hakuna hakuna dini inayotetea ukandamizaji, dhuluma na uovu wa aina yoyote na kwamba Tanzania inawakumbuka watu hao kutokana na historia yake ya kutotambua ubaguzi.
Wananchi wa Tanzania jana Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani waliungana na Waislamu wenzao wa nchi nyingine na kushiriki kwenye maandamano jijini Dar es Salaam ambapo walisisitiza kuendeleza umoja na mshikamano wao na kuunga mkono mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Palestina walio chini ya ukandamizaji wa Wazayuni maghasibu.