Nov 03, 2023 12:27 UTC
  • AU: Juhudi za pamoja zinahitajika kudumisha amani Tigray

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesisitizia haja ya kuwepo jitihada za pamoja kwa ajili ya kudumisha amani katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia na eneo zima la Pembe ya Afrika.

Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Tume ya AU amesema hayo katika taarifa wakati huu ambapo Ethiopia inaadhimisha mwaka mmoja tangu kusainiwa makubaliano ya amani mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Mkataba huo wa amani, uliosimamiwa na Afrika Kusini na Umoja wa Afrika mnamo Novemba 2 mwaka jana, ulihitimisha mapigano ya Tigray ila kutokea wakati huo, kumeibuka machafuko katika sehemu nyingine za nchi hiyo hasa katika jimbo la Amhara.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ameipongeza Ethiopia kwa kudumisha amani, kukumbatia mazungumzo ya kitaifa na kuwa na maridhiano katika eneo la Tigray tokea muafaka huo usainiwe nchini Afrika Kusini mwaka jana.

Utulivu eneo la Tigray

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, ripoti ya Tume ya Kimataifa ya Wataalamu wa Haki za Kibinadamu kuhusu Ethiopia kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa inazituhumu pande zote katika mzozo huo, kwa kutenda ukatili kaskazini mwa Ethiopia.

Kadhalika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeutaka Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuishinikiza serikali ya Ethiopia ili kuhakikisha kwamba wahanga wa vita vya Tigray wanapata haki.

Tags