Mahakama Kuu Uingereza kutoa uamuzi kuhusu uhalali wa kupelekwa Rwanda waomba hifadhi
Mahakama Kuu ya Uingereza wiki ijayo itatoa uamuzi iwapo mpango wa serikali ya nchi hiyo wa kuwapeleka nchini Rwanda, wakimbizi na waomba hifadhi walioko nchini humo ni halali au la.
Uamuzi huo utatolewa baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza kuwasilisha rufaa kupinga uamuzi wa awali wa Mahakama ya Rufaa iliyosema kuwa mpango wa kuwatuma waomba hifadhi nchini Rwanda ni kinyume cha sheria.
Iwapo uamuzi huo utakwenda kinyume cha matarajio ya serikali ya London, Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak, atakuwa chini ya mashinikizo kutoka chama chake ambacho kinataka nchi hiyo ijiondoe kwenye Mkataba wa Ulaya kuhusu haki za binadamu, ECHR.
Majaji watano katika Mahakama Kuu ya Uingereza watatoa uamuzi wao kuhusu pingamizi hilo siku ya Jumatano ijayo.
Mawakili wa serikali wamesema kuwa, Mahakama ya Rufaa haikuwa sahihi kuhitimisha kwamba kupelekwa wahamiaji walioko Uingereza nchini Rwanda kungekiuka kifungu cha 3 cha mkataba wa Ulaya wa haki za binadamu, unaokataza mateso na unyanyasaji au udhalilishaji.

Mpango huo wa serikali ya Uingereza umekuwa ukipingwa vikali na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, wanaosema Rwanda haiwezi kuwa nchi salama kwa wakimbizi na wahamiaji hao.
Iwapo Mahakama Kuu ya Uingereza itahalalisha mpango huo, Wizara ya Mambo ya Ndani inatumai kuwa ndege ya kwanza ya kuwasafirisha wahamiaji inaweza kuanza safari ya kuelekea Kigali mapema mwakani.