Uganda, Sudan Kusini kupambana na wizi wa mifugo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10555-uganda_sudan_kusini_kupambana_na_wizi_wa_mifugo
Serikali za Uganda na Sudan Kusini zimeafikiana kupambana na wizi wa mifugo na haswa ng'ombe unaofanyika mara kwa mara katika vijiji vilivyoko mpakani mwa nchi mbili hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 04, 2016 03:22 UTC
  • Uganda, Sudan Kusini kupambana na wizi wa mifugo

Serikali za Uganda na Sudan Kusini zimeafikiana kupambana na wizi wa mifugo na haswa ng'ombe unaofanyika mara kwa mara katika vijiji vilivyoko mpakani mwa nchi mbili hizo.

Makubaliano hayo yamesainiwa mwezi mmoja baada ya genge la wezi wa mifugo la Sudan Kusini kuvamia eneo la Agoro na Madi-Opei katika wilaya ya Lamwo nchini Uganda na kuiba ng'ombe 44.

Salvatore Abdullah Lorisamoi, Kamishna Mkuu wa jimbo la Imatong nchini Sudan Kusini amesema serikali ya Juba inalaani vikali wizi huo wa mifugo na kwamba iko tayari kushirikiana na nchi zinazopakana nayo ili kukabili wizi huo.

Kwa upande wake, Charles Obong Okwera, Mwenyekiti wa kaunti ndogo ya Madi-Opei nchini Uganda ameitaka serikali ya Sudan Kusini kuheshimu makubaliano hayo kwa shabaha ya kudumisha ujirani mwema na ushirikiano wa pande mbili. Amesema makubaliano ya aina hii yamewahi kuafikiwa mara kadhaa huko nyuma lakini yanakosa kutekelezwa. Alkhamisi iliyopita, viongozi wa kisiasa, kiusalama na kijamii wa nchi mbili hizo jirani walifanya mkutano katika mji wa Lamwo nchini Uganda na kujadili pamoja na mambo mengine, wizi wa mifugo na kuhangaishwa kwa wananchi wa Uganda wanaposafiri kwenda Sudan Kusini.