Waliouawa katika mashambulio ya wabeba silaha Nigeria waongezeka na kufikia 160
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i106434-waliouawa_katika_mashambulio_ya_wabeba_silaha_nigeria_waongezeka_na_kufikia_160
Idadi ya watu waliouawa katika mashambulio yaliyofanywa na makundi ya wabeba silaha kwenye vijiji vya jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria imeongezeka na kufikia 160.
(last modified 2025-10-22T06:10:45+00:00 )
Dec 26, 2023 06:09 UTC
  • Waliouawa katika mashambulio ya wabeba silaha Nigeria waongezeka na kufikia 160

Idadi ya watu waliouawa katika mashambulio yaliyofanywa na makundi ya wabeba silaha kwenye vijiji vya jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria imeongezeka na kufikia 160.

Idadi hiyo ambayo ilitolewa jana Jumatatu, ni kiashiria cha ongezeko la kasi la vifo kutoka idadi ya awali iliyoripotiwa na jeshi Jumapili jioni, ya watu 16 waliokufa katika eneo hilo lililokumbwa na mizozo ya kidini na kikabila kwa miaka kadhaa sasa.

Monday Kassah, mkuu wa serikali ya mtaa katika mji wa Bokkos jimboni Plateau ameviambia vyombo vya habari kuwa, watu wanaokadiriwa kufika 113 wamethibitishwa kuuawa huku mzozo uliozuka Jumamosi ukiendelea hadi alfajiri ya jana Jumatatu.

Kassah amebainisha kuwa, magenge ya kijeshi, yanayojulikana kama majambazi, yalianzisha mashambulizi yaliyoratibiwa katika maeneo ya jamii zisizopungua 20 na kuchoma moto nyumba.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa, walipata zaidi ya watu 300 pia waliojeruhiwa, ambao walihamishiwa hospitali za Bokkos, Jos na Barkin Ladi.

Vilio na simanzi vimetawala katika maeneo yalikotokea mashambulio hayo

Takwimu zisizo rasmi za Shirika la Msalaba Mwekundu zinaonyesha kuwa vifo 104 vimetokea katika vijiji 18 katika eneo la Bokkos.

Takriban watu 50 pia waliripotiwa kufariki katika vijiji kadhaa katika eneo la Barkin Ladi, kulingana na Dickson Chollom, mbunge wa jimbo hilo.

Kwa mujibu wa duru za habari, milio ya risasi iliendelea kusikika hadi jana jioni katika eneo hilo ambalo liko kwenye mstari unaogawanya kaskazini ya Nigeria yenye Waislamu wengi na kusini ambayo wakazi wake wengi ni Wakristo.

Plateau ni mojawapo ya majimbo kadhaa yenye mgawaniko wa kikabila na kidini katika eneo linalojulikana kama Ukanda wa Kati wa Nigeria, ambapo migogoro kati ya jamii tofauti imegharimu mamia ya roho za watu katika miaka ya hivi karibuni.

Vurugu hizo mara nyingi hupewa taswira ya mizozo ya kikabila na kidini kati ya wafugaji Waislamu na wakulima ambao akthari yao ni Wakristo.../