Jan 04, 2024 04:41 UTC
  • Kufungwa ubalozi wa Ufaransa nchini Niger

Hatimaye ubalozi wa Ufaransa umefungwa rasmi nchini Niger miezi kadhaa baada ya kufanyika marekebisho ya kisiasa na Baraza la Kijeshi kuchukua uongozi wa nchi, ambapo lilisisitiza kuondoka vikosi vya kijeshi na kukomeshwa satwa ya Ufaransa katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imetoa taarifa ikisema kuwa umefunga ubalozi wake nchini Niger na kwamba shughuli za ubalozi huo zitaendeshwa kutokea Paris.

Kufungwa ubalozi wa Ufaransa nchini Niger ni tukio la karibuni zaidi katika uhusiano wa nchi hizo na kunaonyesha kusalimu amri  Ufaransa kwa matakwa ya nchi hiyo ya Kiafrika.

Ingawa Ufaransa imekuwepo nchini Niger kwa miongo kadhaa kwa visingizio mbalimbali, hasa madai ya kuimarisha usalama na kupambana na ugaidi katika nchi za eneo la Sahel la Afrika, ikiwemo  Niger na Mali, lakini katika mwaka mmoja uliopita, kufuatia matukio ya kisiasa katika nchi hizo na baadhi ya nchi nyingine za eneo, harakati nyingi zimekuwa zikifanyika dhidi ya uwepo wa wageni katika eneo hilo, hasa Ufaransa.

Kwa hakika, eneo la Sahel ya Afrika, kwa kuwa na rasilimali nyingi za urani na madini mengine ya thamani pamoja na nguvu kazi rahisi, linachukuliwa kuwa la kimkakati la na ndio maana kwa miaka mingi limekuwa kikikodolewa macho na askari wa Kifaransa na raia wa nchi hiyo ya Magharibi. Kwa hakika, viongozi wa Paris katika muongo mmoja uliopita kwa kutumia vibaya matatizo ya kiuchumi na kisiasa pamoja na kuongeza harakati za makundi ya kigaidi katika nchi kama vile Niger wameimarisha uwepo wao kwa kuendesha jinai nyingi barani humo. Kugunduliwa makaburi ya umati karibu na kambi za kijeshi za Ufaransa nchini Mali au kupigwa risasi raia kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi ni ushahidi wa jinai za Ufaransa katika nchi hizo.

Jenerali Abdurrahman Shiani, Mkuu wa Baraza la Kijeshi linalotawala nchini Niger alisema kuhusiana na suala hilo: Wafaransa walikuja kwa kisingizio cha kutokomeza ugaidi, lakini si tu kwamba wameshindwa kupambana na magaidi, bali pia idadi yao imeongeza nchini.'

Maandamano ya wananchi wa Niger dhidi ya uwepo wa Ufaransa nchini humo

Muda tu baada ya kuondolewa madarakani Mohammad Bazum na kuchukua uongozi Baraza la Kijeshi, uondoaji wa vikosi vya jeshi la Ufaransa kutoka nchi hiyo ulipewa umuhimu na kupata uungwaji mkono wa wananchi wa nchi hiyo.

Licha ya juhudi na maombi ya Ufaransa ya kuendelea kubaki katika ardhi ya Niger, hatimaye, kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa liliondoka Niamey wiki chache zilizopita, na hivyo kumaliza duru ya uwepo wa kijeshi  Ufaransa katika nchi hyo ya Kiafrika.

Mkusanyiko wa Waniger mbele ya ubalozi wa Ufaransa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imetangaza kufunga ubalozi wake nchini Niger, ikiwa imepita wiki mbili tokea kuondoka wanajeshi wa Ufaransa katika nchi hiyo. Katika miezi ya karibuni, serikali ya kijeshi ya Niger na wananchi  wa nchi hiyo wamekuwa wakitilia mkazo suala la kuheshimiwa uhuru wao wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi. Kwa hakika, wananchi  wa Afrika, ambao wamekuwa chini ya ubeberu wa nchi nyingi za Ulaya kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja, sasa wanataka wapewe fursa ya kujitawala kikamilifu bila kuingiliwa na nchi za kigeni. Baraza la Kijeshi la Niger limelitaja tukio hilo kuwa mwanzo wa zama mpya kwa wananchi wa Niger. Baraza hilo limeandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa: 'Niger bado iko thabiti na usalama wa ardhi yetu hautawategemea tena  wageni. Tumedhamiria kukabiliana na changamoto zinazotukabili kwa kuimarisha uwezo wetu wa kimkakati, kijeshi na kitaifa.'

Kwa hakika, baada ya miaka mingi ya ukoloni wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja pamoja na uwepo wa wageni, nchi za Kiafrika sasa zimeanza kushuhudia zama mpya za kutegemea nguvu za ndani na kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Nchi hizo kwa kujiamini zinajaribu kujiandalia uwanja mpya na kujichukulia maamuzi yao zenyewe katika mfumo wa kimataifa kinyume na matakwa ya wageni.

Tags