Jan 14, 2024 13:13 UTC
  • Rais Hage Geingob wa Namibia
    Rais Hage Geingob wa Namibia

Namibia imepinga uungaji mkono wa Ujerumani kwa msimamo wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, (ICJ) ambapo inakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Ofisi ya Rais wa Namibia imesema katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba nchi hiyo ina wasiwasi mkubwa kuhusu uamuzi wa kutisha uliotolewa na Ujerumani siku mbili zilizopita, ambapo imepinga mashtaka yaliyowasilishwa na Afrika Kusini mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya Israel.

Ni baada ya Ujerumani kutangaza kuwa itaingilia kati kama upande wa tatu mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuiunga mkono Israel katika kesi ya mauaji ya kimbari iliyowasilishwa dhidi ya utawala huo ghasibu.

Katika taarifa hiyo, Namibia imeashiria mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20, ambayo yalifanywa na Ujerumani katika ardhi ya Namibia kati ya 1904 na 1908, ambapo makumi ya maelfu ya Wanamibia wasio na hatia waliuawa katika mazingira ya kinyama na ya kikatili.

Ujerumani iliuwa makumi ya maelfu ya raia wa Namibia 

Imesema kuwa, serikali ya Ujerumani bado haijafidia kikamilifu mauaji ya kimbari iliyofanya katika ardhi ya Namibia.

Windhoek pia imekosoa msimamo wa Berlin wa kupuuza mashambulizi ya kikatili yaliyosababisha mauaji ya zaidi ya Wapalestina 23,000 huko Gaza na kufumbia macho ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa zinazoangazia kuhama kwa takriban asilimia 85 ya raia huko Gaza huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula na huduma muhimu za kibinadamu.

Ofisi ya Rais wa Namibia imesisitiza wito wa Rais Hage Gottfried Geingob wa nchi hiyo alioutoa mwishoni mwa mwezi uliopita, akisema kuwa "hakuna mtu mpenda amani anayeweza kupuuza mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza."

Rais wa Namibia Hage Geingob ametoa wito kwa serikali ya Ujerumani kufikiria upya uamuzi wake usiofaa wa kuingilia kati kama upande wa tatu kutetea na kuunga mkono vitendo vya mauaji ya kimbari vilivyofanywa na Israel mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Wakoloni wa Ujerumani waliua kwa umati makumi ya maelfu ya watu wa makabila ya Herero na Nama kwenye mauaji ya kuangamiza kizazi yaliyotokea baina ya mwaka 1904 na 1908 ambayo wanahistoria wanayataja kuwa ni mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20.

Tags