Watu 225 wapoteza maisha kutokana na makali ya njaa Tigray, Ethiopia
(last modified Wed, 17 Jan 2024 07:41:52 GMT )
Jan 17, 2024 07:41 UTC
  • Watu 225 wapoteza maisha kutokana na makali ya njaa Tigray, Ethiopia

Watu wasiopungua 225 wameaga dunia katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia kutokana na njaa iliyosababishwa na ukame ambao umeendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Duru za habari zimenukuu mamlaka za eneo hilo zikisema, watu 200 wameaga dunia kwa njaa katika mji wa Edaga Arbi jimboni Tigray tokea mwezi Julai mwaka uliopita hadi sasa.

Aidha watu 16 wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na makali ya njaa katika mji wa Adwa unaopakana na mji huo wa Edaga Arbi jimboni Tigray, wakiwa wahanga wa hivi karibuni wa baa la njaa katika eneo hilo.

Mwezi uliopita wa Disemba, Mshirikishi wa Eneo, Hadush Asemelash aliiambia kanali ya Tigray TV kwamba, watu wasiopungua 176 wakiwemo wanawake 75 wameaga dunia katika eneo la Tigray kutokana na njaa.

Aidha mwezi mmoja kabla ya hapo, yaani Novemba 2023, zaidi ya watu 50 waliripotiwa kuaga dunia katika maeneo ya kaskazini mwa Tigray na Amhara huko nchini Ethiopia kutokana na njaa.

Ukame na kiangazi Ethiopia

Hivi karibuni, Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Ethiopia (EHRC) ilisema wakimbizi zaidi ya 30 wamepoteza maisha kutokana na njaa na utapiamlo katika jimbo la Gambella lililoko magharibi ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Huku maeneo ya kaskazini mwa Ethiopia yakikabiliwa na ukame mkubwa, baadhi ya maeneo ya kusini na mashariki mwa nchi hiyo yanaendelea kusumbuliwa na mvua kubwa za el-Nino na mafuriko.