Jan 25, 2024 03:27 UTC
  • Al-Shabaab yashambulia kambi ya jeshi Somalia, makumi ya askari 'wauawa'

Wanajeshi kadhaa wa Somalia wanahofiwa kuuawa katika shambulizi la kushtukiza la kundi la wanamgambo la al-Shabaab kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wanachama wa kundi hilo la kigaidi jana Jumatano walishambulia kambi ya jeshi katika kijiji cha Caad kilichoko katika mkoa wa kaskazini wa Mudug, na kufanya umwagaji damu mkubwa.

Mamlaka za Somalia bila kutoa maelezo ya kina au kutaja idadi ya wanajeshi wa serikali waliouawa katika shambulizi hilo zimeeleza kuwa, 'pande zote' zimepata hasara kubwa katika makabaliano hayo.

Hii ni katika hali ambayo, genge hilo la kigaidi limetoa taarifa na kudai kuwa limeua wanajeshi 191 baada ya kushambulia kambi hiyo ya kijeshi mkoani Mudug, yenye askari zaidi ya  1,350 wa Jeshi la Taifa la Somalia (SNA).

Al-Shabaab wamezidisha mashambulizi tangu Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud ambaye alichaguliwa kwa muhula wa pili mwaka jana, kutangaza "vita vya hali ya juu" dhidi ya kundi hilo. Wiki iliyopita, genge hilo lilidai kuhusika na mripuko mkubwa uliotikisa wilaya ya Hamarweyne jijini Mogadishu na kuua watu watatu.

Wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab

Genge hilo la kigaidi linafanya mashambulizi haya ili kujaribu kufifiza moto wa operesheni dhidi ya wanachama na ngome zake, wakati huu ambapo Umoja wa Afrika unaendelea kuondoa wanajeshi wa umoja huo (ATMIS) kutoka nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. 

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida linatekeleza mashambulizi ya umwagaji damu huko Somalia tangu mwaka 2007, ili kuiondoa madarakani serikali ya nchi hiyo. 

Tags