9 wafariki dunia katika mkanyagano wakisherehekea Iddi, Ghana
Watu tisa wamepoteza maisha katika mkanyagano wakati wa sherehe za kuadhimisha Sikukuu ya Idul-Fitr jana usiku nchini Ghana.
Habari zinasema kuwa, tisa hao waliaga dunia jana usiku katika mji wa Kumasi kwenye mkanyagano uliotokea baada ya umeme kupotea ghafla na kuzusha taharuki na kuacha kila mmoja akikimbilia usalama wake. Duru zingine za habari zinasema kuwa, baada ya umeme kukatika, mkanganyiko ulijiri baada ya watu waliokuwa wamekusanyika katika ukumbi wa kijamii kukosa hewa kwa kuwa mlango wa ukumbi huo ulikuwa umefungwa. Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, idadi kubwa ya waumini wa Kiislamu waliojeruhiwa katika sherehe hizo za jana usiku wanaendelea kutibiwa katika hospitali na zahanti za mji wa Kumasi, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Jana Jumatano Waislamu katika nchi nyingi duniani walisherehekea Sikukuu ya Idul Fitri inayokamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Sherehe hizo za Idi zilitanguliwa na Swala ya Idul Fitri ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukamilisha ibada adhimu ya funga ambayo ni nguzo ya nne katika dini tukufu ya Kiislamu.