Dola milioni 1.4 zahitajika kukabili homa ya manjano Angola
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema linahitajia dola milioni 1.4 za Marekani ili kukabili maambukizi mapya ya homa ya manjano nchini Angola.
Shirika hilo limesema linahitajia msaada huo wa dharura ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo hatari sio tu katika mikoa 18 ya nchi hiyo, bali katika nchi zingine za Afrika. Red Cross imesema mripuko wa ugonjwa huo ni mbaya mno na haujawahi kushuhudiwa katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Mripuko wa homa ya manjano nchini Angola umesababisha vifo vya watu zaidi ya 350 tangu mwezi Disemba mwaka jana hadi sasa, huku kesi za ugonjwa huo zikienea hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya na hata Uchina. Mripuko wa homa hiyo hatari uligunduliwa kwa mara ya kwanza katika mji mkuu Luanda mwishoni mwa mwaka jana, na hivi sasa kesi za homa hiyo zimeshathibitishwa katika mikoa mingi ya pwani na katikati mwa Angola. Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema katika ripoti yake hivi karibuni kuwa, Angola imesajili jumla ya kesi 3,400 zinazoshukiwa kuwa za homa ya manjano.