Watu 4 wauawa, 40 watekwa nyara kaskazini mwa Nigeria
Kwa wakali watu wanne wameuawa huku makumi ya wengine wakitekwa nyara katika shambulio lililofanywa na kundi moja la wabeba silaha katika jimbo la Zamfara la kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Salisu Ibrahim, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ameliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, wabeba silaha hao jana Jumanne walishambulia mji wa Kasuwa-Daji, katika eneo la Kaura-Namoda na kuanza kufyatua risasi ovyo.
Wakazi wanasema wavamizi hao walikizingira kituo cha polisi katika eneo hilo kwa dakika 30 hivi, kabla ya kuwateka nyara wakazi wasiopungua 40.
Msemaji wa Polisi, Yacid Abubakar amethibitisha habari za kutokea shambulio hilo la wabeba silaha alfajiri ya jana Jumanne jimboni Zamfara. Amesema maafisa usalama wanafanya juu chini kuwaokoa wanakijiji waliotekwa nyara.
Wiki iliyopita, watu wenye silaha waliwateka nyara takriban wanawake 35 waliokuwa wakirejea makwao kutoka kwenye harusi katika jimbo la Katsina, kaskazini-magharibi mwa Nigeria.
Vitendo vya utekaji nyara kwa ajili ya kutaka fidia ni tatizo kubwa nchini Nigeria, na magenge ya wahalifu yanafanya utekaji huo kwenye barabara kuu, majumbani na hata shuleni.
Utekaji nyara ulianza kuwa tatizo kubwa nchini Nigeria mwanzoni mwa milenia ya tatu, lakini wataalamu wanahusisha ongezeko la hivi karibuni la matukio haya na mgogoro wa kiuchumi ambao unayasukuma baadhi ya makundi kufanya vitendo vya uhalifu ili kupata pesa.