Nigeria: Mwezi huu tutatoa ripoti kuhusu mashambulizi ya anga yaliyouwa raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i108648-nigeria_mwezi_huu_tutatoa_ripoti_kuhusu_mashambulizi_ya_anga_yaliyouwa_raia
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jeshi la Nigeria, Jenerali Christopher Musa, amesema kuwa ripoti kuhusu mashambulizi ya anga ya ndege zisizo na rubani (droni) yaliyouwa raia karibu 85 katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi Disemba mwaka jana zitatolewa mwishoni mwa mwezi huu.
(last modified 2024-02-21T11:27:20+00:00 )
Feb 21, 2024 11:27 UTC
  • Nigeria: Mwezi huu tutatoa ripoti kuhusu mashambulizi ya anga yaliyouwa raia

Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jeshi la Nigeria, Jenerali Christopher Musa, amesema kuwa ripoti kuhusu mashambulizi ya anga ya ndege zisizo na rubani (droni) yaliyouwa raia karibu 85 katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi Disemba mwaka jana zitatolewa mwishoni mwa mwezi huu.

Itakumbukwa kuwa Rais Bola Tinubu wa Nigeria aliagiza kufanyika uchunguzi wa kina kufuatia mashambulizi hayo ya droni ambayo yamekuwa yakifanywa kuwalenga wanamgambo wenye silaha na magenge ya wahalifu.

Jeshi la Ulinzi na Kikosi cha Anga cha Nigeria vimetakiwa kukabiliana na vitisho vinavyoongezeka huko kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria kutoka kwa magenge ya wahalifu wenye silaha. Makundi hayo yanayobeba silaha yamekuwa yakifanya  mashambulizi na kutekaji nyara wanavijiji. Jeshi la Nigeria pia linaendesha oparesheni dhidi ya wahalifu huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. 

Wanamgambo wanaobeba silaha Nigeria 

Akizungumza mapema wiki hii na waandishi wa habari huko Abuja, mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Nigeria, Jenerali Christopher Musa, alisema: "Tupo hapa kwa ajili ya kuwalinda raia wa nchi hii, na si kuwashambulia. Kulifanyika makosa, na sasa tunashughulikia kadhia hii." 

Amesema ripoti kuhusu mauaji ya raia 85 yaliyofanywa na ndege zisizo na rubani iko tayari ina inatazamiwa kutolewa kabla ya mwishoni mwa mwezi huu.

tarehe 5 Disemba mwaka jana, Rais Bola Tinubu wa Nigeria aliagiza kufanyika uchunguzi baada ya jeshi la nchi hiyo kukiri kuwa moja ya ndege zake zisizo na rubani (droni) zimeshambulia kwa bahati mbaya kijiji cha Tudun Biri wakati wenyeji wa kijiji hicho walipokuwa wakisherehekea tamasha la Kiislamu.

Wakazi wa kijiji hicho walisema kuwa watu 85 wameuawa wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.