Feb 23, 2024 11:53 UTC
  • Rais Tshisekedi: Niko tayari kusitisha mpango wa kuanzisha vita na Rwanda

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, yuko tayari kusitisha mpango wake wa kuanzisha vita na jirani yake Rwanda, ili kutoa nafasi kwa jitihada zinazoendelea za kupata suluhu ya mzozo unaoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Matamshi yake yamekuja siku chache baada ya Marekani, Ufaransa na washirika wao, kuitaka Rwanda iache kuwasaidia waasi wa M23 na kuondoa wanajeshi wake mashariki mwa nchi hiyo.

Rais wa DRC amesema kuwa, alimwambia Rais Paul Kagame huko Addis Ababa kwamba ni yeye ambaye anahitaji wakutane ana kwa ana ili amuulize swali ili afahamu anataka nini na nchi yake na watu wake.

Rais Tshisekedi amekariri tuhuma zake kwamba Rwanda inajificha nyuma ya kundi la M23, na kuongeza kuwa hiyo ndiyo sababu hawezi kuzungumza na kundi hilo.

Hivi karibuni waasi wa M23 walizidisha mashambulizi yao katika mji wa Sake ambao umekimbiwa na wakazi wake.

Waasii wa M23 ambao inadaiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwamba, wanaungwa mkono na serikali ya Rwanda

 

Ghasia zinazoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinazohusishwa na makundi mbalimbali ya waasi, hasa wa M23, zimesababisha watu wengi kuhama makazi yao, huku mamilioni ya watu wakilazimika kuyahama makazi yao, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu OCHA.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.