Feb 26, 2024 11:46 UTC
  • Baada ya Niger, ECOWAS yaiondolea vikwazo Guinea

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imeamua kuondoa vikwazo ilivyokuwa imeiwekea Guinea.

Ecowas imeeleza hayo katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama uliofanyika katika mji mkuu wa Nigeria Abuja kujadili uamuzi wa mwezi uliopita wa Niger, Mali na Burkina Faso kujiondoa katika jumuiya hiyo ya kikanda ya Afrika Magharibi na mabadiliko ya kisiasa yaliyojiri nchini Senegal.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Guinea baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Septemba 2021 na vikwazo kwa raia wa Mali wanaofanya kazi katika taasisi za ECOWAS vimeondolewa.
 
Kuhusu mgogoro wa kisiasa uliozuka nchini Senegal kufuatia kuakhirishwa uchaguzi a urais ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Februari 25, pande husika katika mgogoro huo zimetakiwa kuyapa kipaumbele maridhiano ili kulinda mafanikio ya kidemokrasia ya nchi hiyo.
Viongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Guinea

Taarifa hiyo pia imesisitiza haja ya kuachiliwa mara moja Rais wa zamani wa Niger Mohamed Bazoum, ambaye amekuwa kizuizini tangu mapinduzi ya Julai 26 mwaka jana.

 
Siku ya Jumamosi iliyopita, ECOWAS ilitangaza kuondoa vikwazo ilivyokuwa imeiwekea Niger vikiwemo vya kuifungia mipaka, kuzuia mali za Benki Kuu na serikali ya nchi hiyo na kusimamisha miamala ya kibiashara na nchi wanachama.
 
Disemba 2023, ECOWAS yenye nchi wanachama 15 ilisimamisha rasmi uanachama wa Niger katika jumuiya hiyo, miezi kadhaa baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi, na kusisitiza kuwa vikwazo hivyo vitaendelezwa hadi utaratibu wa kikatiba utakaporejeshwa nchini humo.../

 

Tags