Mar 22, 2024 02:28 UTC
  • Jiji kuu la Afrika Kusini Johannesburg lakumbwa na uhaba wa maji ambao haujawahi kutokea

Mji mkubwa zaidi wa Afrika Kusini Johannesburg, ambao pia ni mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hiyo umekumbwa na uhaba mkubwa wa maji kwa zaidi ya wiki mbili sasa kutokana na kusambaratika mfumo wake wa maji.

Ripoti kutoka Johannesburg zinasema, wakazi matajiri na maskini wa jiji hilo lenye watu wapatao milioni sita, hawajawahi kushuhudia uhaba mkubwa wa maji kama huo, ambao inaaminika umechangiwa pia na hali ya hewa ya joto iliyosababisha kupungua akiba ya maji kwenye mabwawa.

Hata hivyo, miundombinu inayobomoka na kuharibika baada ya kutelekezwa kwa miongo kadhaa, nayo pia inaaminika kuchangia kushadidi kwa uhaba huo wa maji.

Ripoti iliyochapishwa mwaka jana na Idara ya Taifa ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Afrika Kusini ilionyesha kuwa 40% ya maji yanayotumika katika Manispaa za jiji la Johannesburg yanapotea kupitia uvujaji, unaochangiwa pia na mabomba yaliyopasuka.

Wanaharakati na wakazi wa Johannesburg waliokasirishwa na hali hiyo wanasema, hayo ni matokeo ya kuacha kushughulikia tatizo kwa miaka kadhaa wakilaumu kile wanachokiita usimamizi mbovu wa maafisa husika kwa kushindwa kuifanyia matengenezo mapema miundo msingi ya maji iliyochakaa.

Mwishoni mwa wiki, mamlaka ya usimamizi wa maji katika jimbo la Gauteng, ambalo linajumuisha Johannesburg na mji mkuu, Pretoria, iliwaambia maafisa kutoka miji yote miwili kwamba kushindwa kupunguza kiwango cha matumizi ya maji kunaweza kusababisha mfumo wa maji kusambaratika kikamilifu, kwa sababu hifadhi za maji zingeshuka chini ya uwezo wa 10% na kuhitaji kuzimwa ili kujazwa tena.

Manung'uniko yanayotolewa na wananchi kutokana na tatizo hilo yanaelezewa na wadadisi wa siasa za Afrika Kusini kama ishara ya hatari kwa chama tawala cha African National Congress, ANC ambacho kimekuweko madarakani tangu ulipotokomezwa utawala wa ubaguzi wa rangi katika miaka ya 1990, kutokana na kukabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Mei.../

Tags