Tuhuma za serikali ya Zimbabwe dhidi ya nchi za Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11065-tuhuma_za_serikali_ya_zimbabwe_dhidi_ya_nchi_za_magharibi
Serikali ya Zimbabwe imezituhumu baadhi ya nchi za Magharibi kwamba, zinaunga mkono malalamiko na migomo inayoshuhudiwa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2016 23:15 UTC
  • Tuhuma za serikali ya Zimbabwe dhidi ya nchi za Magharibi

Serikali ya Zimbabwe imezituhumu baadhi ya nchi za Magharibi kwamba, zinaunga mkono malalamiko na migomo inayoshuhudiwa nchini humo.

Dkt. Ignatius Chombo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Zimbabwe amesema kuwa, nyaraka zilizokusanywa na mashirika ya kiintelijensia ya nchi hiyo zinaonesha kuwa, ubalozi wa Ufaransa mjini Harare ukishirikiana na baadhi ya balozi nyingine za kigeni umekuwa na mkono katika mpango wa kutaka kubadilisha utawala wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa waziri huyo ni kuwa, Laurent Delahousse balozi wa Ufaransa na Harry Thomas balozi wa Marekani mjini Harare hivi karibuni walikutana na mchungaji Evan Mawarire mratibu wa malalamiko ya mitaani. Hata hivyo balozi wa Ufaransa mjini Harare amekana tuhuma hizo.

Maandamano na migomo imeyagubika maeneo yote ya Zimbabwe katika siku za hivi karibuni.

Kutoridhishwa raia na hali mbaya ya kiuchumi na kucheleweshwa mishahara yao ni jambo lililopelekea sekta kadhaa kujiunga na mgomo huo wakiwemo walimu, madaktari na wauguzi. Wafanyakazi wa ofisi za serikali nao wameweka chini vifaa vyao vya kazi na kuungana na wimbi la malalamiko kwa ajili ya kuonyesha upinzani wao kwa serikali ya Rais Robert Mugabe.

Filihali, harakati za kiuchumi nchini Zimbabwe zimesimama huku shule, hospitali na maduka yakiwa yamefungwa. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, katika mazingira haya ambapo hali ya kiafya ya Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 92 haieleweki huku chama chake cha ZANU-PF kikivutana mashati kuhusiana na nani atakayemrithi Mugabe, kuna uwezekano kwamba, nchi hiyo inaelekea katika vurugu na machafuko ya ndani.

Kile ambacho kwa sasa kimevuta hisia na masikio ya wengi barani Afrika ni malalamiko ya wananchi wa Zimbabwe dhidi ya sera mbovu za kiuchumi za Rais Mugabe ambazo hazijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 36 ya utawala wake wa kidikteta. Kwa sasa wananchi wa Zimbabwe wana hamasa kubwa ya kumiminika katika barabara na mitaa ya mji mkuu Harare ili kulalamikia sera za serikali ya nchi yao. Mbali na kuzorota uchumi hali ambayo imeifanya serikali ishindwe kuwalipa mishahara wafanyakazi wake, Zimbabwe inaandamwa na athari mbaya zilizoachwa na ukame ulioikumba nchi hiyo.

Baadhi ya wataalamu wa mambo wanasema kuwa, mpango wa marekebisho ya ardhi ulioanza kutekelezwa na serikali mwaka 2000 ulikuwa mwanzo wa kuporomoka uchumi wa nchi hiyo. Huko nyuma kipindi fulani Zimbabwe ilikuwa maarufu kwa jina la "Kikapu cha Mkate' barani Afrika.

Viongozi wa chama tawala cha Zanu-pf wanaendelea kumuunga mkono Rais Mugabwe huku wakitumia nguvu kuyakandamiza maandamano ya wananchi ili kuzima sauti ya malalamiko. Katika siku za hivi karibuni polisi ya kutuliza fujo ilitumia nguvu kuwatawanya waandamanaji.

Pamoja na hayo mgomo unaohusisha matabaka mbalimbali ya wananchi nchini humo ni jambo linaloonesha mara hii wananchi hao hawako tayari kuachana kwa urahisi na msimamo wao.

Hata hivyo kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, mara hii pia Rais Mugabe anataka kuonyesha kuwa, madola ya Magharibi yanafanya njama za kuiangusha serikali yake.

Marekani, Uingereza na Ufaransa zinahesabiwa kuwa wapinzani wakuu wa Mugabe tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1980 na Mugabe kuchukua hatamu za uongozi. Hata hivyo utendaji wa Mugabe na chama chake cha Zanu-pf katika uchaguzi wa mwaka 2008 ambapo kwa mara ya kwanza Morgan Tsvangirai wa chama cha upinzani alipata ushindi, ulithibitisha kwamba, mrengo huo tawala katu hauna nia ya kuacha madaraka yachukuliwe na chama kingine.

Rais Mugabe na wafuasi wake wananadi kwamba, matatizo ya sasa ya Zimbabwe ni urithi wa mkolobni; hata hivyo hivi sasa imepita takribani nusu karne tangu nchi nyingi za Kiafrika zijipatie uhuru na ni vigumu kudhani kwamba, shida na umasikini wa Waafrika chimbuko lake pekee ni siasa za kidhulma za wakoloni. Ufisadi serikalini, sera mbovu, kung'ang'ania madaraka na uchu wa kujilimbikizia utajiri wa watawala wa sasa barani Afrika ambao hawako tayari kuachia madaraka, ni matatizo mengine yanayozikabili nchi nyingi za Kiafrika ikiwemo Zimbabwe.