Raia wa Uganda wazuiwa kutembelea Sudan Kusini
Jeshi la polisi la Uganda jana liliwapiga marufuku raia wa nchi hiyo kutembelea Sudan Kusini baada ya kuzuka mapigano mapya katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba na kupelekea watu wasiopungua 300 kuuawa.
Msemaji wa jeshi la polisi ya Uganda, Fred Enanga amenukuliwa na toleo la leo la gazeti la Daily Monitor la nchi hiyo akisema mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za jeshi hilo huko Naguru, jijini Kampala kwamba mkutano wa pamoja wa polisi, jeshi na mashirika mengine ya usalama ya Uganda umeamua kuwa raia wa Uganda wapigwe marufuku kwenda nchini Sudan Kusini kutokana na hali mbaya ya kiusalama katika nchi hiyo.
Huku hayo yakiripotiwa, wafanyabiashara wasiopungua watano raia wa Uganda waliuawa jana jioni katika mapigano yanayoendelea baina ya askari watiifu kwa Rais wa Salva Kiir wa Sudan Kusini na wale wa makamu wake, Riek Machar.
Watu walioshuhudia wamesema kuwa, mauaji hayo yalitokea katika eneo la Aruu ndani ya Sudan Kusini saa kumi jioni, jana Jumatatu. Mashuhuda wanasema, gari lililokuwa na watu kumi lilishambuliwa kwenye eneo hilo wakati lilipokuwa linatoka Juba kuelekea kwenye eneo la mpakani la Elegu.