Kiongozi wa harakati ya upinzani akamatwa Zimbabwe
Mkuu wa harakati inayoongoza malalamiko na upinzani wa wananchi dhidi ya utendaji wa serikali ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametiwa nguvuni kwa tuhuma za kuchochea wananchi.
Harrison Nkomo ambaye ni wakili wa kiongozi wa harakati ya malalamiko ya wananchi, Evan Mawarire, amesema mteja wake amekamatwa leo.
Maandamano ya wananchi wa Zimbabwe yaliyoanza wiki mbili zilizopita kupinga utendaji wa serikali ya Rais Mugabe yangali yanaendelea hadi sasa. Maandamano hayo yamekwamisha shughuli mbalimbali za idara za serikali, mahakama, maduka, shule na kadhalika.
Wachunguzi wa Taasisi ya Kidemokrasia ya Zimbabwe wanasema kuwa, kuna uwezekano mkubwa nchi hiyo ikatumbukia katika machafuko na ukosefu wa amani kwa kutilia maanani hali isiyojulikana ya kiafya ya Rais Robert Mugabe anayeingoza nchi hiyo tangu ilipopata uhuru na vilevile vita vya kuwania madaraka ndani ya chama tawala cha ZANU-PF.