May 05, 2024 06:43 UTC
  • UN yaonya kuhusu njaa huko Darfur ikiwa pande zinazozozana hazitaruhusu msaada kuingia

Shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa limeonya kuhusu hatari ya njaa huko Darfur iwapo pande zinazozozana hazitaruhusu msaada kuingia katika eneo hilo la magharibi mwa Sudan.

WFP inasema kuongezeka mapigano katika mji mkuu wa Darfur Kaskazini, El Fasher, kunazuia juhudi za kupeleka msaada muhimu wa chakula katika eneo hilo.

Raia katika mji huo na eneo pana la Darfur tayari wanasumbuliwa na kiwango kikubwa cha njaa, lakini uwasilishaji wa msaada wa chakula umekuwa wa kusuasua kutokana na vikwazo vya ukiritimba na mapigano yanayoendelea katika maeneo hayo.

Sudan

Sudan imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, tangu mvutano unaoendelea kati ya jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka ulipoanza, Aprili 2023.

Kushadidi ghasia na mapigano katika mji El Fasher kumesitisha misafara ya misaada kutoka kwenye kivuko cha mpaka cha Tine cha Chad, kilichofunguliwa hivi karibuni kwa ajili ya misaada ya kibinadamu.

Msemaji wa WFP nchini Sudan, Leni Kinzli, ametoa wito wa kuruhusiwa misaada ya kibinadamu kuelekea katika maeneo yenye mizozo nchini Sudan na kusema: Tunahitaji dhamana ya usalama ili kutoa usaidizi kwa familia zinazohangaika ili kunusurika.