May 07, 2024 02:16 UTC
  • Wananchi wa Chad wasubiri matokeo baada ya uchaguzi wa rais jana

Wananchi wa Chad wanasubiri kwa hamu matokeo ya uchaguzi wa Rais uliofanyika jana (Jumatatu) ambao ulisusiwa na mrengo wa upinzani.

Wananchi wa Chad Jumatatu ya jana walipiga kura katika uchaguzi wenye lengo la kumaliza miaka mitatu ya utawala wa kijeshi lakini uliosusiwa na wapinzani wa kiongozi wa kijeshi Mahamat Idriss Deby.

Matokeo ya uchaguzi huo yanatajiwa kuamua ikiwa wananchi wa Chad wanataka kuongeza miongo mitatu ya utawala wa familia ya Deby, katika nchi hiyo muhimu katika vita dhidi ya uasi katika eneo la jangwa la Sahel au la.

Mpinzani mkuu kwenye kinyang’anyiro cha rais ni waziri mkuu Succes Masra, anayeshtumiwa na wakosoaji kuwa kibaraka kwa kutokuwepo wapinzani wengine wakubwa.

Wagombea wote wawili wameapa kushinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo, ambao mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yanaonya kuwa hautakuwa huru au wa haki

Rais mtarajiwa Mahamat Idriss Deby akipiga kura katika uchaguzi wa jana Jumatatu (05.05.2024)

 

Uchaguzi huu wa Chad unafuatia kura ya maoni ya katiba iliyofanyika tarehe 17 Desemba 2023, kufuatia kifo cha Rais Idriss Déby mwaka wa 2021.

Mahamat Idriss Deby alichukua mamlaka mnamo 2021 baada ya kifo cha baba yake, Idriss Deby Itno, ambaye alikufa kwenye mstari wa mbele wa vita dhidi ya waasi baada ya kutawala kwa miaka 30.

Anawania kwa tiketi ya chama tawala cha Patriotic Salvation Movement (MPS), kilichoasisiwa na babake, na anaungwa mkono na muungano wa vyama vingine zaidi ya 200.