Kiongozi wa harakati ya malalamiko apandishwa kizimbani Zimbabwe
Kiongozi wa harakati ya malalamiko ya wananchi nchini Zimbabwe ya Stay at Home amepandishwa kizimbani kujibu mashtaka ya kuchochea ghasia na kuhatarisha usalama wa nchi.
Pastor Evan Mawarire alifikishwa mahakamani leo mjini Harare chini ya ulinzi mkali wa polisi wa kuzuia ghasia.
Harakati ya upinzani inayoongozwa na Pastor Evan Mawarire inahesabiwa kuwa kubwa zaidi dhidi ya serikali ya Rais Mugabe katika miaka ya hivi karibuni.
Makumi ya wanaharakati waliokuwa wakitoa nara dhidi ya serikali ya Zimbabwe walizuiliwa nje ya mahakama hiyo.
Wakati huo huo shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, kutiwa mbaroni kwa Pastor Evan Mawarire ni harakati inayofanyika kwa mpangilio maalumu kwa ajili ya kuwatia woga wanaharakati wa kambi ya upinzani.
Amnesty imesema kuwa, badala ya kukandamiza sauti za wapinzani, serikali ya Zimbabwe inapaswa kutegea sikio matakwa na malalamiko yao.
Wananchi wa Zimbabwe wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga ughali wa maisha, kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira, ufisadi ndani ya taasisi za serikali na kadhalika.