Jul 14, 2016 07:20 UTC
  • Kutokuwa na natija duru mpya ya mazungumzo ya amani ya Burundi

Duru mpya ya mazungumzo ya amani ya Burundi kwa usimamizi wa Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa imeshindwa kuwa na matunda kutokana na makundi ya upinzani kulalamikia kushiriki katika mazungumzo hayo viongozi kadhaa wa serikali ya Bujumbura.

Zaidi ya wawakilishi 70 wa makundi mbalimbali ya kisiasa, asasi za kijamii na kidini za Burundi walishiriki katika duru hiyo ya pili ya mazungumzo.

Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilifanyika tarehe 21 hadi 24 za mwezi Mei mwaka huu ambayo nayo haikuwa na natija kutokana na kutohudhuria mazungumzo hayo muungano mkuu wa upinzani.

Duru ya pili ya mazungumzo ya amani ya Burundi imevunjika katika hali ambayo, weledi wa mambo wanaamini kwamba, mazungumzo ndio njia pekee ya kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo.

Burundi ilitumbukia katika kinamasi cha mgogoro wa kisiasa Aprili mwaka jana kufuatia hatua ya chama tawala nchini humo cha CNDD-FDD ya kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea urais kwa muhula wa tatu katika uchaguzi uliopita. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, tamaa ya kuendelea kubakia madarakani Rais Nkurunziza ndio chimbuko la kile kinachoshuhudiwa hii leo nchini Burundi. Mbali na mamia ya watu kuuawa tangu machafuko hayo yaibuke, kuna raia laki mbili na nusu wa nchi hiyo ambao wamelazimika kuikimbia nchi yao na kuwa wakimbizi.

Hivi sasa hatua ya Rais Nkurunziza ya kung'ang'ania madaraka kwa upande mmoja na ukiukwaji wa haki za binadamu na mateso dhidi ya wapinzani kwa upande mwingine, ni mambo ambayo yamezidi kuwa na taathira hasi kwa nchi hiyo.

Ripoti mbalimbali za Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch zimelaani vitendo vya mateso vinavyofanyika nchini Burundi kwa malengo na msukumo wa kisiasa. Aidha mauaji yanayowalenga viongozi wa serikali ambapo tukio la karibuni kabisa ni la kuuawa Hafsa Mossi Mbunge wa Afrika Mashariki na aliyewahi kuwa Waziri wa Burundi katika Jumuiya ya EAC ambaye alipigwa risasi hapo jana, ni matukio ambayo yamezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wananchi.

Alaa kulli haal, filihali wananchi wa Burundi wanalazimika kuubeba mzigo mzito waliotwishwa wa kiu ya madaraka ya Nkurunziza.

Hati ya makubaliano ya Arusha Tanzania ya Agosti mwaka 2000 iliyotiwa saini kati ya serikali na makundi yenye silaha ya Wahutu ilihesabiwa kuwa fremu ya kimsingi kwa ajili ya kurejesha amani nchini Burundi. Kwa mujibu wa hati hiyo, rais wa nchi hapaswi kuongoza kwa zaidi ya duru mbili.

Hata hivyo Nkurunziza ambaye anatoka kabila la Wahutu amekiuka hati ya makubaliano ya Arusha na kama wanavyosema wachambuzi wa mambo ni kuwa, hatua yake hiyo ndiyo iliyoitumbukiza Burundi katika mgogoro wa kisiasa wa hivi sasa.

Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, kuendelea mgogoro wa Burundi kutakuwa tishio kubwa kwa eneo zima la Maziwa Makuu.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekuwa zikifanya juhudi za kusimamia mazungumzo ya amani ya nchi hiyo kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro huo ambao unatishia kuibua tena vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo.

Tags