Jeshi la Uganda laanza kuondoa raia wake Sudan Kusini
Msafara wa magari ya jeshi la Uganda umeingia Sudan Kusini na kuanza kuwaondoa maelfu ya raia wa nchi hiyo waliokwama mjini Juba kutokana na mapigano mapya yaliyoikumba nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Malori 50 ya Jeshi la Ulinzi la Uganda UPDF yaliyokuwa na askari waliojizatiti kwa silaha yameingia Sudan Kusini kupitia mji wa Nimule, yapata kilomita 200 kaskazini mwa kituo cha mpakani kwa shabaha ya kuwaondoa raia 3,000 wa nchi hiyo mjini Juba. Taarifa ya serikali ya Kampala imesema kikosi hicho chenye askari wapatao 2,000 kitajishughulisha tu na kuhakikisha kuwa raia wa Uganda wanarejea nyumbani salama salmin. Brigedia Leopold Kyanda, kamanda mwandamizi wa jeshi la Uganda amesema zoezi hilo litafanyika kwa muda wa siku kama 3 hivi. Haya yanajiri siku chache baada ya Msemaji wa UPDF, Luteni Kanali Paddy Ankunda kukanusha madai kuwa Uganda inajiandaa kutuma wanajeshi wake huko Sudan Kusini kama ilivyofanya mwezi isemba mwaka 2013, kwenda kudhibiti mambo katika mji mkuu Juba. Hii ni katika hali ambayo, Rais Barack Obama wa Marekani ameidhinisha kutumwa askari 47 wa nchi hiyo kwa ajili ya kulinda ubalozi wa Marekani mjini Juba. Kadhalika Ujerumani na Italia zimeanza kuwaondoa raia wao nchini Sudan Kusini kutokana na kushtadi mapigano hayo. Mapigano baina ya wafuasi wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na makamu wake Riek Machar mjini Juba, yamepelekea zaidi ya watu 300 kuuawa na maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao. Baadhi ya duru za habari zinasema idadi ya waliouawa katika mapigano hayo yaliyoanza Alkhamisi iliyopita yumkini imepindukia watu 1,000.