Ripoti: 90% ya migogoro iliyopuuzwa duniani ipo Afrika
Shirika moja la kibinadamu limesema aghalabu ya migogoro iliyotelekezwa duniani ipo katika nchi za bara Afrika.
Ripoti mpya ya Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) inasema kuwa, asilimia 90 ya migogoro ambayo ilisahaulika na kuupuzwa mwaka uliopita 2023 ilisajiliwa katika eneo la Sahel na eneo la Kati barani Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Burkina Faso inaongoza katika orodha ya nchi hizo, ikifuatiwa na Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mali na Niger. Honduras ambayo ipo katika eneo la Amerika ya Kati ndiyo nchi pekee isiyo ya Afrika katika orodha hiyo.
Nchi nyingine za Kiafrika ambazo zinakamilisha orodha ya mataifa 10 duniani yenye migogoro iliyotelekezwa zaidi duniani ni Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad na Sudan.
Kwa mujibu wa vigezo vya NRC, maeneo yenye migogoro iliyopuuzwa ni maeneo ambayo changamoto zao haziakisiwa ipasavyo na vyombo vya habari, watunga sheria na sera hawatoi kipaumbele katika kupatia ufumbuzi matatizo, na nchi wafadhili hazitiyapi maeneo au nchi hizo misaada na fedha za kutosha.
Ripoti zinaonyesha kuwa, migogoro na ghasia duniani zilisababisha ongezeko la kushtua la idadi ya wakimbizi wa ndani hasa barani Afrika mwaka uliopita 2023.
Katika nchi za Afrika, eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara, idadi ya wakimbizi wa ndani iliongezeka zaidi ya maradufu kutoka watu milioni 16.5 mwaka 2018 hadi watu milioni 34.8 mwishoni mwa 2023.