Jun 12, 2024 11:23 UTC
  • Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa DR Congo aapishwa

Bi Judith Suminwa Tuluka ameapishwa kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Tuluka na wajumbe wengine 54 wapya wa serikali wamechukua madaraka baada ya wabunge kuidhinisha mpango wa utekelezaji wa Tuluka kwa wingi kamili wa kura.

Wakati akiwasilisha mpango na ratiba yake ya utendaji Jumanne mchana, alisema anajivunia kuvunja "dari ya kioo" na kuwa mwanamke wa kwanza wa Kongo kutumikia nchi akiwa Waziri Mkuu.

Amesema: "Kwa kushika nafasi hii, ninafahamu kikamilifu umuhimu wa kihistoria wa wakati huu na sbabu za uteuzi huu kwa taifa la Kongo."

Aidha ametumia fursa hiyo kutangaza msingi wa "Kongo inayostawi" kwa kuandaa ajira zipatazo milioni 2.6 na chuo cha hisabati na Akili Mnemba yaani Artificial Intelligence (AI) mjini Kinshasa. Vile vile ametangaza hatua atakazochukua za kulinda usalama wa taifa, kuimarisha uchumi, kuunganisha miundombinu, huduma za umma, na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akiwa na shahada ya uzamili ya uchumi aliyosomea kwenye Chuo Kikuu cha Universite libre de Bruxelles nchini Ubelgiji, Tuluka amewahi kutumikia serikali ya DRC kama waziri wa serikali wa masuala ya mipango mnamo Machi 2023. Kuanzia 2020 hadi 2023 aliwahi kuwa naibu mratibu wa Baraza la Rais la Ufuatiliaji wa Mikakati, taasisi ambayo iko chini ya ofisi ya rais.

Serikali hii mpya DRC iliyozinduliwa Mei 29, ina wajumbe 55, akiwemo waziri mkuu, manaibu waziri mkuu sita, na mawaziri 10 wa majimbo.

Tags