Jeshi la Rwanda lapinga madai ya kuwabaka wanawake Jamhuri ya Afrika ya Kati
(last modified 2024-10-17T10:45:33+00:00 )
Oct 17, 2024 10:45 UTC
  • Jeshi la Rwanda lapinga madai ya kuwabaka wanawake Jamhuri ya Afrika ya Kati

Jeshi la Rwanda limekanusha madai ya ubakaji dhidi ya wanajeshi wake wanaohudumu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), likisema kuwa wanajeshi wa Rwanda katika ujumbe huo ni "wastaarabu" na "wanalinda na kuheshimu watu wanaokutana nao".

Gazeti la New Humanitarian liliripoti jana Jumatano jinsi wanawake na wasichana katika Jamhuri ya Afrika ya Kati "wanavyoendelea kutishiwa" na unyanyasaji wa kijinsia na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, na wengi wanakaa kimya "kwa hofu ya kulipiziwa kisasi". Takriban wanawake wanne wanawatuhumu wanajeshi sita wa Rwanda, wawili kati yao wakiwa nchini humo chini ya makubaliano ya ushirikiano wa pande mbili, na wengine katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaojulikana kama MINUSCA.

Jeshi la Rwanda linasema kwamba, vituo vya jeshi la Rwanda katika Jamhuri ya Afrika ya Kati haviruhusu kuingia kwa raia ambao hawakuja kwa njia inayojulikana, "ili kusiwe na unyanyasaji wa raia katika kituo hicho".

Miongoni mwa wanaotuhumiwa kwa vitendo hivyo ni pamoja na vikosi vya Rwanda, Burundi na Zambia ambavyo ni sehemu ya ujumbe unaojulikana kwa jina la MINUSCA pamoja na wapiganaji wa zamani wa Kundi la Wagner ambao ni sehemu ya makubaliano ya ushirikiano wa nchi hizo.

Waasi wa zamani wa SELEKA katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

 

Gazeti la New Humanitarian linasema vikosi vya kijeshi vya nchi zote zilizotajwa hazijatoa maoni yoyote juu ya mashtaka dhidi ya askari wao.

Rwanda ina jeshi la ngazi mbili katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, lile lililo katika ujumbe wa MINUSCA na lile lililo katika makubaliano ya usaidizi yaliyotiwa saini kati ya Kigali na Bangui mwishoni mwa 2019, ambayo yaliwezesha jeshi la Rwanda kutetea utawala wa Rais Faustin- Archange Touadéra ambayo ilirejeshwa na waasi wakiongozwa na rais wa zamani François Bozizé.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2015 kumekuwa na zaidi ya visa 730 vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa huko Afrika ya Kati.

Tags