Wakulima wa Afrika Kusini watuhumiwa kuuwa wanawake 2, na kisha miili yao kuwalisha nguruwe
(last modified 2024-09-11T03:12:19+00:00 )
Sep 11, 2024 03:12 UTC
  • Wakulima wa Afrika Kusini watuhumiwa kuuwa wanawake 2, na kisha miili yao kuwalisha nguruwe

Wanaume watatu nchini Afrika Kusini wanatuhumiwa kuwauwa wanawake wawili na kisha miili yao kuwalisha nguruwe katika shamba lao. Kesi hii tajwa imeibua ghadhabu na hasira miongoni mwa jamii ya Afrika Kusini.

Wanaume hao watatu jana walifikishwa mahakamani katika jimbo la kaskazini la Limpopo. Serikali imewataka watuhumiwa kusalia gerezani hadi kesi yao itakapokamilika.

Zacharian Johannes Olivier, mmiliki wa shamba, msimamizi, Andrian Rudoloh de Wet na mfanyakazi William Musora wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kuua kwa kukusudia, moja la kujaribu kuua na kukutwa na silaha isiyo na kibali. 

Musora ambaye ni raia wa Zimbabwe pia anakabiliwa namashtaka ya kuishi Afrika Kusini kinyume cha sheria.  

Inadaiwa kuwa mnamo mwezi Agosti mwaka huu, lori la kampuni moja ya maziwa lilitupa bidhaa katika shamba la Olivier ambazo muda wake wa matumizi ulikuwa umekwisha na kisha  wanawake waliotajwa kwa majina ya Locadia Ndlovu na Maria Makgatho baadaye walianza kukusanya bidhaa hizo. Hata hivyo shambani hapo wanawake hao wawili walipigwa risasi na kuuawa. Mwanaume aliyekuwa pamoja na wanawake hao alijeruhiwa na kutambaa hadi kwenye barabara iliyo karibu ili kupiga mayowe ya kuomba msaada. Baadaye polisi ilikuta miili ya wanawake hao ikiwa imeoza katika banda la nguruwe. 

Vyama kadhaa vya kisiasa jana viliandamana nje ya Mahakama ya Mankweng, vikitaka watu hao wanyimwe dhamana na wakabiliwe na adhabu kali zaidi. 

Uhalifu wa kikatili katika mashamba ya Afrika Kusini umekuwa suala lenye kuibua wasiwasi kwa miaka mingi sasa, ikiwa ni pamoja na kuuliwa ovyo wakulima na  wakulima kwa wafanyakazi wao. Kesi hii tajwa itaendelea mwezi ujao. 

Tags