Balozi: Nchi 18 zimejiunga na kesi ya Afrika Kusini ICJ dhidi ya Israel
(last modified 2024-10-08T11:41:27+00:00 )
Oct 08, 2024 11:41 UTC
  • Balozi: Nchi 18 zimejiunga na kesi ya Afrika Kusini ICJ dhidi ya Israel

Balozi wa Afrika Kusini mjini Tehran, Dakta Francis Moloi, ameashiria kuongezeka kwa uungaji mkono wa kimataifa kwa kesi ya mauaji ya kimbari ya Gaza dhidi ya Israel, akieleza kuwa kufikia sasa nchi 18 zimejiunga na kesi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ.

Katika mahojiano na shirika la habari la Tasnim, Dakta Francis Moloi amezungumzia vita vya Israel huko Gaza, uungaji mkono wa Afrika Kusini kwa haki za Wapalestina, na kesi ya kisheria inayoendelea dhidi ya mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.

Mwanadiplomasia huyo wa Afrika Kusini amelinganisha namna Israeli inavyowafanyia ukatili Wapalestina na uzoefu wa Afrika Kusini katika utawala wa ubaguzi wa rangi wa apartheid, akisisitiza mshikamano kati ya mapambano hayo mawili.

Katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel ICJ mwaka jana, mahakama hiyo kuu ya Umoja wa Mataifa ilitoa maamuzi matatu ya muda mnamo Januari 26, Machi 28 na Mei 24.

Mawakili na wanaharakati wa Afrika katika mahakama ya ICJ

ICJ iliiamuru Israel kuchukua hatua zote ndani ya uwezo wake kuzuia mauaji ya kimbari huko Gaza, kuruhusu upatikanaji wa chakula bila vikwazo katika eneo la Palestina lililozingirwa, na kusitisha mara moja uvamizi wake wa kijeshi katika mji wa kusini wa Rafah. Israel imepuuza maagizo hayo yote ya ICJ.

Katika kuadhimisha mwaka mmoja wa vita huko Gaza, Rais wa Afrika Kusini jana Jumatatu alisema nchi yake itawasilisha faili jipya baadaye mwezi huu ICJ, lenye ithibati na ushahidi wa kuthibitisha kuwa Israel inatekeleza uhalifu wa mauaji ya halaiki huko Palestina.

Tags