Jun 17, 2024 07:10 UTC
  • Magaidi wa JNIM: Tumehusika na shambulio lililoa askari 107 Burkina Faso

Kundi la kigaidi la Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limetangaza kuwa wapiganaji wake ndio waliofanya shambulio la hivi karibuni lilililoua makumi ya wanajeshi wa Burkina Faso.

Kundi la kiitelijensia la SITE jana Jumapili lilinukuu taarifa ya genge hilo la kigaidi likikiri kuwa, wanamgambo wake walishambulia kambi ya kijeshi katika mji wa Mansila ulioko katika mkoa wa Yagha, mpakani na Niger na kuua wanajeshi 107 wa Burkina Faso siku tano zilizopita.

Video kadhaa zilizosambazwa mitandaoni na kundi hilo la wabeba silaha zinaonesha wapiganaji wa genge hilo wakishambulia kwa risasi kambi hiyo, na kisha kutwaa makumi ya silaha na zana za kijeshi. Aidha zinaonesha wanajeshi saba wa Burkina Faso waliotekwa na genge hilo.

Machi mwaka huu, Aly Benjamin Coulibaly, Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Burkina Faso alieleza kuwa watu takriban watu 170 waliuawa katika mashambulizi dhidi ya vijiji vitatu katika jimbo la Yatenga kaskazini mwa nchi hiyo mwishoni mwa Februari.

Magaidi Burkina Faso

Kwa muongo mmoja sasa, Burkina Faso imekuwa ikikabiliana na uhalifu na machafuko yanayosababishwa na wanamgambo wanaobeba silaha wenye mfungamano na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na ISIS (Daesh) ambao walisambaratika kutoka nchi jirani ya Mali mwaka 2015.

Magenge hayo yanayojinasibisha na Uislamu, yamekuwa yakishambulia hata misikiti na kuua Waislamu. Hivi karibuni, makumi ya waumini wa Kiislamu waliuawa katika shambulizi dhidi ya msikiti nchini Burkina Faso, siku ambayo watu 15 waliuawa pia katika hujuma nyingine dhidi ya kanisa nchini humo.

Tags