Jun 24, 2024 06:51 UTC
  • ANC: Vyama 10 vya kisiasa kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Afrika Kusini

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress (ANC) kimetangaza kuwa vyama 10 vya kisiasa vyenye viti Bungeni vimekubali kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na ANC (GNU).

Katika taarifa yake, chama cha ANC kimesema: "Baada ya wiki mbili za mazungumzo makali, vyama 10 kati ya 18 vyenye viti katika Bunge la Taifa vimeonesha nia yao ya kushirikiana nasi katika GNU ili kuleta ustawi kwa watu wa Afrika Kusini."

Vyama hivyo 10 ni pamoja na ANC, Democratic Alliance, Patriotic Alliance, Inkatha Freedom Party, GOOD, Pan Africanist Congress of Azania, Freedom Front Plus (Vryheidsfront Plus), United Democratic Movement, Rise Mzansi na Al Jama-ah.

Kwa pamoja, vyama hivyo vilipata zaidi ya asilimia 70 ya kura katika uchaguzi wa 2024, na vitaifanya serikali ya GNU kuwa na wingi mutlaki katika Bunge la Afrika Kusini na kuiwezesha kupitisha miswada kiurahisi.

Chama cha ANC kimesema: Vyama hivyo vimekubaliana na kanuni za msingi za kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kufanikisha malengo ya GNU.

Aidha chama hicho tawala cha Afrika Kusini kimesema kuwa, kitaendelea kufanya mawasiliano ya wazi na vyama vingine ambavyo havijajiunga na GNU.

Katika uchaguzi mkuu wa Mei 29, ANC ilipata viti 159 kati ya 400 vya Bunge na kushuka chini ya asilimia 50 inayohitajika kuwa na wingi mutlaki ambao ilikuwa nao kwa muda wa miaka 30 katika bunge hilo.