Watu 7 wauawa, 100 watekwa nyara kaskazini mwa Nigeria
Genge moja la wabeba silaha limevamia kijiji kimoja huko kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuua watu wasiopungua saba, mbali na kuteka nyara makumi ya wengine.
Polisi nchini Nigeria wamethibitisha kuwa watu zaidi ya 100 wametekwa nyara na watu wenye silaha katika uvamizi huo dhidi ya kijiji cha Maidabino katika jimbo la kaskazini magharibi la Katsina.
Msemaji wa Polisi katika jimbo la Katina, Abubakar Aliyu Sadiq ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, kundi hilo la wahalifu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha lilishambulia kijiji hicho Jumamosi asubuhi, na kutekeleza unyama huo.
Naye Hassan Aliyu, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, aghalabu ya wanakijiji waliotekwa nyara katika shambulio hilo ni wanawake, watoto wadogo na vijana.
Habari zaidi zinasema kuwa, wavamizi hao walifunga barabara zote za kuingia katika kijiji hicho kabla ya kuanza kuwafyatulia risasi wakazi wa kijiji hicho.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu sita kuuawa huku zaidi ya 100 wakitekwa nyara na majambazi waliokuwa na silaha katika uvamizi mwingine dhidi ya kijiji cha Tudun Doki, wilaya ya Gwadabawa katika jimbo la kaskazini magharibi la Sokoto.
Magaidi, majambazi na magenge ya wabeba silaha mara kwa mara hushambulia vijiji, shule na taasisi za kielemu na kuwateka nyara watu hasa wanafunzi nchini Nigeria. Mara nyingi wanadai fidia ili kuwaachilia huru mateka wao.