Jul 16, 2016 06:46 UTC
  • WHO: Maambukizi ya homa ya manjano DRC yaongezeka kwa 38%

Shirika la Afya Duniani WHO lilisema kuwa kesi za maambukizi mapya ya ugonjwa hatari wa homa ya manjano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeongezeka kwa asilimia 38 katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.

Yokouide Allarangar, mwakilishi wa WHO nchini Kongo amesema kufikia Julai 11, kesi 1,798 za ugonjwa huo zilikuwa zimerikodiwa kutoka kesi 1,307 zilizonakiliwa Juni 24. Amesema watu 75 wanaaminika kuaga dunia kutokana na ugonjwa huo kufikia sasa katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Mwezi uliopita, serikali ya DRC ilitangaza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya manjano umeukumba mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa ambao una idadi ya watu zaidi ya milioni 10 na miji mingine miwili ya magharibi mwa Kongo. Waziri wa Afya wa Kongo, Kabange Numbi alisema kesi 68 za maambukizi ya homa ya manjano zikiwemo za watu 5 kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo, zimethibitishwa katika mikoa ya Kinshasa, Kongo ya Kati na Kwango. Ameongeza kuwa, kesi nyingi za ugonjwa huo zimehusishwa na mlipuko wa homa ya manjano katika nchi jirani ya Angola ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 350 tangu mwezi Disemba mwaka jana.

Hivi karibuni, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema kuwa ugonjwa wa homa ya manjano ulioripuka nchini Angola sasa umeenea katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya na hata Uchina.

Tags