Takriban wahamiaji 89 wamefariki dunia baada ya mtumbwi kupinduka pwani ya Mauritania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113734-takriban_wahamiaji_89_wamefariki_dunia_baada_ya_mtumbwi_kupinduka_pwani_ya_mauritania
Mtumbwi mmoja uliokuwa na wahamiaji haramu umepinduka katika fukwe za Mauritania na kusababisha vifo vya wahamiaji 89. Mtumbwi huo ulikuwa unaelekea barani Ulaya na watu walioshuhudia wanasema kuwa, ulikuwa na abiria 170.
(last modified 2024-07-05T23:06:51+00:00 )
Jul 05, 2024 23:06 UTC
  • Takriban wahamiaji 89 wamefariki dunia baada ya mtumbwi kupinduka pwani ya Mauritania

Mtumbwi mmoja uliokuwa na wahamiaji haramu umepinduka katika fukwe za Mauritania na kusababisha vifo vya wahamiaji 89. Mtumbwi huo ulikuwa unaelekea barani Ulaya na watu walioshuhudia wanasema kuwa, ulikuwa na abiria 170.

Shirika la habari la serikali ya Mauritania limetangaza habari hiyo na kusema kwamba, watu hao walikuwa wanasafiri kwa kutumia mtumbwi wa kienyeji wa kuvulia samaki, kujaribu kuvuka Bahari ya Atlantiki yenye mawimbi makali. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, makumi ya wengine hawajulikani walipo hadi hivi sasa baada ya ajali hiyo iliyotokea Julai 1, 2024 katika mji wa Ndiago wa kusini magharibi mwa Mauritania.

Shirika hilo la habari limewanukuu watu walionusurika wakisema kuwa, mtumbwi huo ulikuwa umesheheni abiria na ulianzia safari yake katika mpaka wa Senegal na Gambia ukiwa na abiria 170.

Wavuvi wanaokodiwa na magenge ya magendo ya binadamu kusafirisha watu kinyume cha sheria

 

Taarifa ya serikali ya Mauritania imesema kuwa, hadi wakati wanatangaza habari hiyo, maafisa wa serikali walikuwa wameshaokoa watu tisa. Mmoja wa walionusurika kifo ni msichana wa miaka mitano.

Sasa hivi kuna ulinzi mkali katika Bahari ya Mediterania hivyo magenge ya kusafirisha binadamu kimagendo barani Afrika yameamua kutumia Bahari ya Atlantiki kusafirisha watu kuelekea barani Ulaya kwa tamaa chapwa ya kupata maisha bora. Njia hiyo ni hatari mno hasa kutokana na mikondo yake mikubwa na mawimbi makali.

Pia, wahamiaji hao mara nyingi hushehenezwa kwenye mitumbwi au mashua zilizojaa watu kupita kiasi, wakati mwingine hazina hata maji ya kutosha ya kunywa. Kawaida vyombo hivyo huwa havina vifaa vya usafari salama.