Ramaphosa: Afrika Kusini itaendelea kuimarisha uhusiano na Iran
(last modified Wed, 10 Jul 2024 14:56:55 GMT )
Jul 10, 2024 14:56 UTC
  • Ramaphosa: Afrika Kusini itaendelea kuimarisha uhusiano na Iran

Viongozi wa nchi mbalimbali duniani akiwemo Rais wa Afrika Kusini wameendelea kumpongeza Rais mteule wa Iran, Massoud Pezeshkian kwa kuibuka na ushindi katika duru ya 14 ya uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu.

Katika ujumbe wake wa pongezi, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema nchi hiyo ina hamu ya kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga mbali mbali.

Ramaphosa amenukuliwa na shirika la habari la Mehra akisema kuwa, kuimarisha zaidi uhusiano mzuri, wa muda mrefu na uliokita mizizi wa pande mbili ni kwa maslahi ya wananchi wa Afrika Kusini na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wakati huo huo, Rais Nicolus Maduro wa Venezuela sanjari na kumpongeza Pezeshkian kwa ushindi wake, amesema serikali yake itaendelea kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Maduro (kushoto) na Dakta Pezeshkian

Maduro katika mazungumzo ya simu na Dakta Pezeshkian, sambamba na kuipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uchaguzi uliofanikiwa, amewasifu wananchi wa Iran walioshiriki uchaguzi huo kwa wingi ili kuzima njama za maadui dhidi ya umoja wao.

Kadhalika Rais mteule wa Iran amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Pashinyan ambaye ameipongeza Iran kwa kufanikisha uchaguzi, akibainisha kuwa nchi hiyo ina hamu ya kunyanyua juu zaidi kiwango cha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili.

Kwa upande wake, Dakta Pezeshkian amesema Tehran inapinga mpango wowote wa kubadilisha mipaka ya kimataifa. Wawili hao wameeleza hamu ya mataifa haya mawili ya kuboresha mahusiano yao kwa kutekeleza hati za ushirikiano zilizosainiwa huko nyuma, na kusaini makubaliano mapya.

Tags