Uongozi wa kijeshi wa Mali waidhinisha upya shughuli za kisiasa
Serikali ya kijeshi ya Mali imeamua kuidhinisha upya shughuli za vyama na harakati za kisiasa nchini humo. Utawala wa Mali mapema mwaka huu ulisimamisha shughuli za vyama vya kisiasa baada ya vyama na harakati za kisiasa za nchi hiyo kutuhumiwa kuendesha mijadala ya upotoshaji.
Uongozi wa kijeshi wa Mali jana ulitangaza kuruhusu tena shughuli za vyama na harakati za kisiasa nchini humo na kuondoa marufuku uliyoiweka mwezi Aprili mwaka huu. Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka Baraza la Mawaziri la Mali linaloongozwa na viongozi wa kijeshi waliochukua madaraka kupitia mapinduzi ya mwaka 2020.
Kanali Assimi Goita mkuu wa serikali ya kijeshi ya Mali mwezi Aprili mwaka huu aliagiza kusimamishwa kwa shughuli za vyama na harakati za kisiasa nchini humo akivikosoa kwa kuendesha mijadala tasa na ya upotoshaji ambayo alisema ilikuwa hatari kwa mazungumzo ya kitaifa yaliyokuwa yakiendelea kuhusu mustakbali wa kisiasa wa Mali.
Vyama vya kisiasa nchini Mali wakati huo vilikuwa vikipinga uamuzi wa makanali wa kusalia madarakani baada ya kumaliza muhula ulioainishwa wa Machi 2024 ili kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kiraia.
Itakumbukuwa kuwa vyama vikuu vya upinzani nchini Mali vilisusia mazungumzo ambayo hata hivyo yaliendelea kufanyika kwa kuungwa mkono na wafuasi wa utawala wa kijeshi ambao mwezi Mei ulipendekeza kuwa wanajeshi wabaki madarakani "kwa miaka miwili hadi mitano ya ziada", na kwamba mkuu wa sasa wa serikaliya kijeshi aruhusiwe kugombea katika uchaguzi wowote ujao wa urais.