Burkina Faso yatangaza kupiga marufuku vitendo vya ushoga
Utawala wa kijeshi nchini Burkina Faso umeidhinisha muswada wa kupiga marufuku vitendo vya ushoga na usagaji.
Kwa mujibu wa ofisi ya rais, mkutano wa baraza la mawaziri umeidhinisha mpango huo unaopiga marufuku vitendo vilivyo kinyume na maumbile vya mapenzi ya watu wa jinsia moja.
Bila ya kuweka wazi adhabu itakayotolewa kwa wahusika wa vitendo hivyo, Waziri wa Sheria Edasso Rodrigue Bayala ameeleza kuwa ushoga na vitendo vinavyohusiana na matukio hayo vitaadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Muswada huo unatarajiwa kuwa sheria baada ya kuidhinishwa na wabunge katika bunge la mpito ambalo limekuwa likitumika tangu kutokea kwa mapinduzi mawili ya kijeshi mwaka wa 2022 katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Mwezi Agosti mwaka uliopita, shirika la uangalizi wa vyombo vya habari nchini humo lilipiga marufuku televisheni zilizodaiwa kuhusika na vitendo vya kupigia debe ushoga. Vitendo vya ushoga ni kinyume cha sheria katika nchi 30 za Afrika, ikiwemo Ghana na Uganda ambazo hivi karibuni zilitangaza sheria kali dhidi ya ushoga. Hatua ya mataifa hayo kupiga marafuku vitendo hivyo imelaaniwa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu na mataifa ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani, pamoja na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, mataifa hayo yanasisitiza kuwa, vitendo hivyo hivyo vichafu vya kufanya mapenzi watu wa jinsia moja vinakwenda kinyume na maumbile ya mwanadamu na utamaduni wa Kiafrika.