Mauzo ya nje ya kahawa yaiingizia Ethiopia dola bilioni 1.43
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113962-mauzo_ya_nje_ya_kahawa_yaiingizia_ethiopia_dola_bilioni_1.43
Uuzaji wa kahawa nje ya nchi umeiletea Ethiopia mapato ya dola bilioni 1.43 katika mwaka wa fedha uliomalizika hivi karibuni.
(last modified 2024-07-12T03:05:31+00:00 )
Jul 12, 2024 03:05 UTC
  • Mauzo ya nje ya kahawa yaiingizia Ethiopia dola bilioni 1.43

Uuzaji wa kahawa nje ya nchi umeiletea Ethiopia mapato ya dola bilioni 1.43 katika mwaka wa fedha uliomalizika hivi karibuni.

Serikali ya Addis Ababa kupitia Mamlaka ya Kahawa na Chai ya Ethiopia (ECTA) imesema katika ripoti yake ya karibuni kabisa kwamba, mwaka ulioisha wa fedha wa 2023/24 uliomalizika mwezi Julai 7, Ethiopia iliuza nje tani 298,500 za kahawa.

Ripoti ya ECTA imeongeza kuwa: Mwezi Juni pekee, nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika iliuza nje tani 46,000 za kahawa, na hivyo kuvunja rekodi ya dola milioni 218 katika mapato yake.

Takwimu za ECTA zinaonyesha kuwa kiasi cha kahawa iliyouzwa nje ya Ethiopia katika mwaka wa fedha wa 2023/24 kilipanda kwa takriban asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita.

 

Ethiopia, ni chimbuko la kahawa ya Arabica na ni moja ya wazalishaji na wauzaji wakubwa wa bidhaa hiyo barani Afrika. Uzalishaji wa kahawa ni kama uti wa mgongo wa uchumi wa nchi hiyo unaotegemea kilimo.

Kahawa ya Ethiopia ina washitiri wengi dunia kutokana na ubora wake na ladha yake ya kipekee.

Hata hivyo wakulima wa buni hawafaidiki inavyotakiwa huko Ethiopia. Wataalamu mara nyingi wanasema kuwa, sababu kubwa ni uuzaji wa malighafi badala ya Ethiopia kusindika yenyewe kahawa. Wanasema hicho ni kikwazo kikubwa kinachozuia Ethiopia kufaidika kikamilifu na rasilimali zake nyingi za kahawa, kwani inasafirisha zaidi buni kwenye soko la kimataifa badala ya kahawa yenyewe.