Mashirika ya misaada: Mamilioni ya Wakongo hawajafikiwa na misaada
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113992-mashirika_ya_misaada_mamilioni_ya_wakongo_hawajafikiwa_na_misaada
Wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu na makundi ya kiraia wanasema kuwa, mamilioni ya watu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo bado hawajafikiwa na misaada licha ya mapigano kusitishwa kwa wiki mbili.
(last modified 2024-07-12T22:43:50+00:00 )
Jul 12, 2024 22:43 UTC
  • Mashirika ya misaada: Mamilioni ya Wakongo hawajafikiwa na misaada

Wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu na makundi ya kiraia wanasema kuwa, mamilioni ya watu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo bado hawajafikiwa na misaada licha ya mapigano kusitishwa kwa wiki mbili.

Wafanyakazi hao wameziambia duru za habari kwamba, kipindi hicho cha wiki mbili ambacho wiki moja tayari imeshakwisha kamilika, hakitoshi.

Afisa wa ngazi za juu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Abdoulaye Barry, amesema kwamba licha ya amri hiyo ya usitishwaji mapigano, kumekuwa na ripoti za machafuko katika eneo la Masisi karibu na makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini.

Mapigano makali kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali yamesababisha wimbi jipya la wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Duru mbalimbali katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini zimeripoti kuhusiana na wimbi hilo jipya la wakimbizi.

Mwezi Januari mwaka huu Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza kuanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Maendelezo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC dhidi ya waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.