WHO: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inakabiliwa na janga la kiafya
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inakabiliwa na janga hatari la kiafya na kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.
Taarifa ya WHO inaeleza kuwa, magonjwa ya milipuko yamezorotesha sana hali ya kiafya nchini humo katika miezi ya hivi karibuni kutokana na ghasia na mafuriko.
Kulingana na WHO, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekabiliwa na ongezeko la migogoro na ghasia, na kusababisha watu wengi kukimbia makazi yao, magonjwa kuenea, unyanyasaji wa kijinsia, na kiwewe kikubwa cha akili, haswa mashariki mwa nchi hiyo.
Dkt. Adelheid Marschang, Afisa wa Dharura wa WHO, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva kwamba "Kutokana na hali hiyo, watu wanakabiliwa na milipuko ya ugonjwa wa kipindupindu, surua, uti wa mgongo, ndui na tauni, yote yakichangiwa na mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yanayoathiri sehemu kadhaa za nchi hiyo."
Aidha Shirika la Afya Duniani linasema kuwa, zaidi ya watoto milioni moja wako katika hatari ya utapiamlo uliokithiri huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku ghasia zikiongezeka na kuongeza mahitaji miongoni mwa mamilioni ya watu wasiokuwa na makazi.
Athari kwa raia kutokana na mzozo wa zaidi ya miaka miwili kati ya jeshi la Congo na wanamgambo wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo zinazidi kuwa mbaya, na kusababisha watu wengi zaidi kukimbia huku milioni 2.7 wakiwa hawana makazi huko Kivu Kaskazini pekee.