Senegal kuangalia upya mikataba ya mafuta na gesi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114066-senegal_kuangalia_upya_mikataba_ya_mafuta_na_gesi
Serikali ya Senegal imetangaza kuwa, itaangalia upya mikataba ya mafuta na gesi iliyotiwa saini na mataifa mbalimbali.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 14, 2024 23:17 UTC
  • Bassirou Diomaye Faye
    Bassirou Diomaye Faye

Serikali ya Senegal imetangaza kuwa, itaangalia upya mikataba ya mafuta na gesi iliyotiwa saini na mataifa mbalimbali.

Hayo yameelezwa na Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye ambaye amesisitiza kwamba, nchi yake inapanga kutathmini na kujadili upya mikataba yake ya mafuta.

Rais Faye amesema hayo baada ya kutimiza siku 100 madarakani na kuongeza kuwa, mikataba hiyo ingeweza kuwa bora na yenye manufaa zaidi kwa taifa lake.

Kiongozi huyo wa Senegal aliyeshinda urais katika uchaguzi wa mwezi Machi mwaka huu, aliagiza ukaguzi ufanyike katika sekta za mafuta na gesi baada ya kuingia madarakani.

Aidha amebainisha kuwa, majadiliano mapya ya mikataba hiyo yanalenga kuleta manufaa kwa pande zote zinazohusika na mikataba hiyo.

Kauli ya Rais Faye imetolewa baada ya kampuni ya mafuta ya Australia ya Woodside Energy kutangaza kuwa machimbo yake ya mafuta na gesi ya Sangomar yamezalisha mafuta kwa mara ya kwanza nchini humo na kuifanya Senegal kuwa mzalishaji mpya wa mafuta duniani.

Hata hivyo, kampuni hiyo inamiliki asilimia 82 ya hisa za mradi huo wakati kampuni ya mafuta ya taifa ya Senegal Petrosen ikiwa na asilimia 18 tu za hisa.

Kwa mujibu wa serikali mpya ya Senegal chini ya uongozi wa Rais Faye, kuna mikataba katika sekta ya mafuuta na gesi ambayo inahatarisha maslahi ya taifa na rasilimali za nchi hiyo.