Wanyarwanda wapiga kura kuchagua rais na wawakilishi wao bungeni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114074-wanyarwanda_wapiga_kura_kuchagua_rais_na_wawakilishi_wao_bungeni
Mamilioni ya Wanyarwanda leo wameelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua rais na wawakilishi wao bungeni.
(last modified 2024-07-15T03:02:08+00:00 )
Jul 15, 2024 03:02 UTC
  • Wanyarwanda wapiga kura kuchagua rais na wawakilishi wao bungeni

Mamilioni ya Wanyarwanda leo wameelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua rais na wawakilishi wao bungeni.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda (NEC), zaidi ya Wanyarwanda milioni tisa wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo utakaoamua Rais na Wabunge kwa muhula ujao wa miaka mitano.

Wanyarwanda milioni mbili kati yao wanapiga kura kwa mara ya kwanza.

Wagombea watatu wanachuana kuwania kiti cha rais wa Rwanda. Paul Kagame wa RPF-Inkotanyi anayeongoza Rwanda kwa kipindi cha miaka 24, anachuana na wagombea wenzake wawili, Frank Habineza wa Democratic Green Party of Rwanda na Philippe Mpayimana, ambaye ni mgombea huru.

Katika upande wa uchaguzi wa Bunge wagombea 589 wachuana kuwania viti 80 vya Bunge la Rwanda. Wanajumuisha wagombea wanaowakilisha vyama vya siasa, wale wanaowakilisha makundi maalumu (vijana, wanawake na watu wenye ulemavu) pamoja na mgombea mmoja huru.

Zaidi ya waangalizi 1,100 wa ndani na nje wameidhinishwa kusimamiai uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda, Oda Gasinzigwa, amesema matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais yatatangazwa leo usiku, wakati yale ya uchaguzi wa Bunge yataanza kutangazwa kesho Jumanne.

Matokeo ya mwisho ya chaguzi za leo nchini Rwanda yatatangazwa Julai 27.

Wakosoaji wanasema wapinzani wakuu wa Rais Paul Kagame kama Diane Rwigara, wamezuiwa kushiriki katika uchaguzi huo.