Miili zaidi yagunduliwa kwenye magunia Nairobi, taharuki yatanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114078-miili_zaidi_yagunduliwa_kwenye_magunia_nairobi_taharuki_yatanda
Kugunduliwa mili zaidi ya watu ikiwa imefungwa kwenye magunia jijini Nairobi nchini Kenya kumezidisha taharuki na kuibua kitendawili cha nani amehusika na vifo au muaji hayo.
(last modified 2024-07-15T04:20:50+00:00 )
Jul 15, 2024 04:20 UTC
  • Miili zaidi yagunduliwa kwenye magunia Nairobi, taharuki yatanda

Kugunduliwa mili zaidi ya watu ikiwa imefungwa kwenye magunia jijini Nairobi nchini Kenya kumezidisha taharuki na kuibua kitendawili cha nani amehusika na vifo au muaji hayo.

Katika hatua mpya, maafisa wote katika Kituo cha Polisi cha Kware, Embakasi, jijini Nairobi, kilichoko karibu na timbo ambapo maiti nane zimeopolewa tangu Ijumaa iliyopita, wamehamishwa eneo hilo huku uchunguzi kuhusu kisa hicho ukiendelea.

Kaimu Ispekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin jana walitangaza kuwa wapelelezi watahitaji angalau muda wa siku 21 kufichua kilichotokea katika eneo la tukio lililoko eneo bunge la Embakasi Kusini.

Bw Kanja amesema kuhamishwa polisi hao kutatoa nafasi kwa maafisa wa upelelezi kuandaa ripoti ya haki na isiyopendelea upande wowote. 

“Nimewahamisha maafisa wote wa polisi waliokuwa wakihudumu katika Kituo cha Polisi cha Kware. Wakati kama huu mgumu tunasimama na jamii ya eneo hilo na tumejitolewa kufichua ukweli na kuhakikisha kuwa wahusika wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Ispekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.

Ameongeza kuwa, kufikia sasa, mshukiwa mmoja ametambuliwa na anachunguzwa na polisi.

Kwa upande wake, kurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin amesema miili hiyo imeoza kwa kiwango tofauti, japo yote ilikatakatwa na kuwekwa ndani ya magunia.

Mohamed Amin: Wote ni wanawake

Mohamed Amin amesema: “Mbinu iliyotumika ni moja. Miaka yao ni kati ya 18 hadi 30. Wote ni wanawake. Na miili hiyo imepakiwa na kufungwa kwa njia sawa.”

Bw Amin alisema mauaji hayo ya kiajabu yamechangia kuibuliwa kwa nadharia nyingi kuhusu kile kilichochochea unyama huo.