25 wauawa, kujeruhiwa Somalia wakitazama fainali ya EURO 2024
Kwa akali watu watano wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika shambulio la bomu linaloaminika kufanywa na kundi la kigaidi la al-Shabaab huko Mogadishi, mkuu wa Somalia.
Msemaji wa Jeshi la Polisi la Somalia, Meja Abdifatah Aden Hassan amesema mbali na watu watano kuuawa, wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa vibaya baada ya kutokea mripuko wa bomu katika mkahawa mmoja mjini Mogadishu.
Amesema waliouawa na kujeruhiwa walikuwa wamekusanyika kwenye mkahawa mmoja jana usiku kwa ajili ya kutazama mchuano wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya (EURO2024) kati ya Uhispania na Uingereza.
Uhispania imetwaa kombe hilo baada ya kuicharaza Uingereza mabao 2-1 kwenye fainali hiyo ya aina yake iliyopigwa katika Uwanja wa Olimpiki wa Berlin nchini Ujerumani.
Msemaji wa Jeshi la Polisi la Somalia ameeleza kuwa, hujuma ya jana ndilo shambulio kubwa zaidi kutokea katika miezi ya karibu huko Mogadishu, mji ambao ulikuwa umeshuhudia utulivu na amani kwa miezi kadhaa sasa. Mohamed Yusuf, afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Somalia kwa upande wake amesema waliouawa katika shambulio hilo lajana usiku ni watu 9.
Genge la kigaidi la al-Shabaab linaonekana kupunguza mashambulizi yake tangu Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud kutangaza "vita vya kila namna" dhidi ya genge hilo.
Kampeni hiyo inaonekana imefanikiwa kiasi kwamba, hivi sasa kikosi cha ATMIS cha Umoja wa Afrika kinaendelea na mchakato wa kuondoa askari wake nchini humo ili kukabidhi masuala yote ya ulinzi kwa vikosi vya serikali ya Somalia.